WHO Yatuma Tani 11 za Vifaa Muhimu Kukabiliana na Ebola DRC
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetuma tani 11 za vifaa muhimu vya matibabu kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika jimbo la Ituri nchini Democratic Republic of the Congo (DRC).
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Mei 19, WHO imesema hatua hiyo ni sehemu ya mwitikio wa haraka wenye lengo la kudhibiti kusambaa kwa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo baada ya mlipuko huo kutangazwa rasmi.
WHO ilieleza kuwa ndani ya saa 72 tangu kutangazwa kwa mlipuko huo Mei 15, 2026, tayari ilikuwa imefanikisha usafirishaji wa tani 11.5 za vifaa muhimu vya kitabibu kutoka vituo vyake vya dharura vilivyopo Kinshasa, Dakar pamoja na Nairobi.
Vifaa vilivyotumwa vinajumuisha mavazi maalumu ya kujikinga kwa wahudumu wa afya, vifaa vya matibabu, mahema ya huduma za dharura pamoja na vifaa vya maji, usafi na mazingira salama (WASH).
Picha zilizotolewa na WHO zinaonesha wafanyakazi wa shirika hilo wakisimamia upakiaji wa vifaa hivyo vya Ebola kwenye ndege iliyokuwa ikielekea DRC kutoka Nairobi mnamo Mei 19, 2026.
WHO pia imesema imekuwa ikishirikiana kwa karibu na mashirika mengine pamoja na sekta binafsi kuhakikisha vifaa vya dharura vinafika kwa haraka katika maeneo yaliyoathirika.
Miongoni mwa washirika waliohusika ni United Nations Organization Stabilization Mission in the Democratic Republic of the Congo (MONUSCO), ambayo ilitoa msaada wa usafiri wa anga na ardhini, huku Ethiopian Airlines ikibadilisha ratiba za safari zake ili kuharakisha usafirishaji wa mizigo hiyo kutoka Nairobi kuelekea DRC.





Post a Comment
Related Discussions...