Wizara yajibu kuhusu Marekani kutuma wagonjwa walioathiriwa au waliokaribiana na maambukizi ya Ebola nchini Kenya
Wizara ya Afya nchini Kenya imetoa uhakikisho kwa wananchi kuwa taifa hilo liko tayari kukabiliana na tishio lolote la ugonjwa wa Ebola, kufuatia taarifa zinazoeleza kuwa Marekani inaweza kutuma wagonjwa walioathiriwa au waliokaribiana na maambukizi ya Ebola nchini humo kwa ajili ya uangalizi maalum na matibabu.
Kupitia taarifa iliyotolewa Mei 27, wizara hiyo haikuthibitisha moja kwa moja uwepo wa mpango huo, lakini ilisisitiza kuwa Kenya itaendelea kufuata sheria zake za kitaifa, kanuni za usalama wa kibayolojia pamoja na viwango vya afya ya umma ili kuhakikisha usalama wa wananchi, wahudumu wa afya na jamii kwa ujumla.
Wizara hiyo ilisema serikali ya Kenya inaendelea na majadiliano na serikali ya Marekani pamoja na washirika wengine wa kimataifa kuhusu ushirikiano wa kuimarisha maandalizi na hatua za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola pamoja na vitisho vingine vya afya vinavyojitokeza duniani.
Aidha, serikali imeeleza kuwa ushirikiano wowote wa kimataifa kuhusu afya utaongozwa na sheria za Kenya, kanuni za afya ya umma, viwango vya usalama wa kibayolojia na jukumu kuu la kulinda afya na ustawi wa wananchi wa Kenya.
Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale, amesema nchi hiyo tayari imechukua hatua mbalimbali za kujiandaa dhidi ya hatari ya kuenea kwa Ebola.
Hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Dharura za Afya (IMS), kuimarishwa kwa uchunguzi katika maeneo yote ya mipakani na viwanja vya ndege, kutengwa kwa maabara maalum za upimaji pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti.
Wizara hiyo pia ilisisitiza kuwa Kenya inaunga mkono ushirikiano wa kimataifa unaolenga kuimarisha usalama wa afya duniani na kulinda maisha ya watu kupitia hatua za kisayansi na ushirikiano wa pamoja.



Post a Comment