Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa ni Ebola vimegundulika DR Congo - WHO
JChanzo cha picha,AFP
Zaidi ya visa 900 vinavyoshukiwa kuwa Ebola, ikiwemo visa 101 vilivyothibitishwa, vimegunduliwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, siku ya Jumapili.
Haya yanajiri baada ya wakazi wenye hasira katika mji ulio katika kitovu cha mlipuko wa Ebola mashariki mwa Kongo kushambulia na kuchoma hema lililokuwa sehemu ya kituo cha afya kinachotibu wagonjwa wa virusi hivyo, wahudumu wa afya wamesema Jumamosi. Tukio hilo lilikuwa la pili la aina hiyo katika eneo hilo ndani ya wiki moja.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulio hilo, lakini wagonjwa walipokimbia ili kuepuka moto huo, watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa Ebola walitoroka katika kituo hicho na hadi sasa hawajulikani walipo, alisema mkurugenzi wa hospitali ya eneo hilo.
Wakazi hao wenye hasira walifika katika kliniki iliyopo katika mji wa Mongbwalu usiku wa Ijumaa na kuchoma moto hema lililokuwa limewekwa kwa ajili ya wagonjwa wanaoshukiwa na waliothibitishwa kuwa na Ebola, lililokuwa likiendeshwa na shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), alisema Dk. Richard Lokudi, mkurugenzi wa hospitali ya Mongbwalu, akizungumza na shirika la habari la Associated Press.
“Tunalilaani vikali tukio hili, kwani limesababisha hofu miongoni mwa wahudumu na pia kusababisha kutoroka kwa watu 18 wanaoshukiwa kuambukizwa katika jamii,” alisema.
Siku ya Alhamisi, kituo kingine cha matibabu katika mji wa Rwampara kilichomwa moto baada ya ndugu wa marehemu kuzuiwa kuchukua mwili wa mwanafamilia wao aliyeshukiwa kufariki kutokana na Ebola. Via Bbc.





Post a Comment
Related Discussions...