Bots Waipiku Binadamu Mtandaoni, AI Yatikisa Mustakabali wa Tovuti

Matumizi ya mifumo ya akili bandia (AI) na bots yamefikia kiwango kipya duniani baada ya takwimu za hivi karibuni kuonyesha kuwa mashine sasa zinazalisha trafiki kubwa zaidi ya internet kuliko binadamu.

Kwa mujibu wa kampuni ya ulinzi wa mifumo ya wingu, Cloudflare, mifumo ya kiotomatiki kwa sasa inachangia takriban asilimia 57.5 ya trafiki yote ya internet duniani, huku binadamu wakichangia asilimia 42.5 pekee.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Matthew Prince, amesema kasi ya ukuaji wa trafiki inayotokana na AI imekuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa. Alieleza kuwa awali alitarajia bots kuipita trafiki ya binadamu mwaka 2027, lakini maendeleo ya haraka ya teknolojia ya AI yamesababisha hatua hiyo kufikiwa mapema zaidi.

Ingawa binadamu bado hutumia muda mwingi zaidi mtandaoni kwa shughuli kama kutazama video, kusoma habari na kutumia mitandao ya kijamii, bots huzalisha maombi mengi ya haraka kwa seva za internet, jambo linaloongeza kiwango cha trafiki kwa kasi kubwa.

Mabadiliko hayo yanaibua changamoto kadhaa kwa wamiliki wa tovuti. Kwanza, ongezeko la bots linaongeza matumizi ya bandwidth na rasilimali za seva, hali inayoweza kusababisha gharama kubwa za uendeshaji au hata kufanya baadhi ya tovuti kushindwa kuhudumia watumiaji ipasavyo.

Pili, matumizi ya AI katika kutafuta na kuchakata taarifa yanaweza kupunguza idadi ya wageni wanaotembelea tovuti moja kwa moja. Badala ya kufungua tovuti, watumiaji wanaweza kupata majibu kupitia mifumo ya AI, jambo linaloweza kupunguza mapato yanayotokana na matangazo na idadi ya wasomaji kwa wachapishaji wa maudhui mtandaoni.

Wataalamu wa teknolojia wanaamini kuwa mwenendo huu utaendelea kukua katika miaka ijayo, huku kampuni nyingi zikitafuta njia mpya za kulinda maudhui yao na kuhakikisha zinaendelea kupata mapato katika enzi ambayo AI inazidi kuwa sehemu muhimu ya matumizi ya internet.

Reply

Discussions