Iran Yapata Ruhusa ya Kuingia Marekani kwa Kombe la Dunia 2026

Timu ya taifa ya Iran imepata afueni baada ya wachezaji wake kuidhinishiwa visa vya kuingia Marekani kwa ajili ya kushiriki Kombe la Dunia la FIFA 2026, linalotarajiwa kufanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.

Balozi wa Marekani nchini Uturuki, Tom Barrack, amethibitisha hatua hiyo akiwapongeza maafisa wa ubalozi wa Marekani mjini Ankara kwa kushughulikia kwa mafanikio maombi ya visa ya kikosi hicho. Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Barrack alisema michezo ina uwezo wa kuunganisha watu wa mataifa mbalimbali licha ya tofauti za kisiasa na migogoro inayoweza kuwepo.

Kwa mujibu wa ratiba ya maandalizi, kikosi cha Iran kinatarajiwa kuondoka Uturuki kuelekea Hispania kabla ya kusafiri kwenda Mexico, ambako kimechagua kuweka kambi yake rasmi wakati wa mashindano hayo. Serikali ya Mexico tayari imekamilisha taratibu za kuwaruhusu wachezaji hao kuingia nchini humo.

Awali Iran ilikuwa imepanga kuweka makazi yake ndani ya Marekani, lakini hali ya mvutano wa kisiasa kati ya Tehran na Washington imeifanya timu hiyo kubadili mpango huo na kuhamishia kambi yake nchini Mexico.

Licha ya kuweka kambi Mexico, mechi zote za hatua ya makundi za Iran zitachezwa nchini Marekani. Timu hiyo itaanza safari yake ya Kombe la Dunia kwa kukutana na New Zealand Juni 16 jijini Los Angeles. Baadaye itacheza dhidi ya Belgium katika jiji hilo hilo kabla ya kumalizia mechi za makundi kwa kuivaa Egypt mjini Seattle.

Uamuzi wa kuruhusu wachezaji wa Iran kuingia Marekani umeonekana kama ishara kwamba michezo inaweza kuendelea kuwa jukwaa la kuleta watu pamoja hata katika nyakati ambazo mahusiano ya kisiasa kati ya nchi yanapitia changamoto kubwa.

1 Comments

Post a Comment

Discussions