Head

Kombe la Dunia 2026 Kuanza Rasmi Mexico Leo

Mashabiki wa soka duniani leo wanaelekeza macho yao nchini Mexico ambapo michuano ya Kombe la Dunia 2026 inaanza rasmi kwa mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Mexico dhidi ya Afrika Kusini katika uwanja maarufu wa Estadio Azteca uliopo jijini Mexico City.

Mashindano hayo yanayotarajiwa kuvutia mabilioni ya watazamaji duniani ni ya kwanza kufanyika katika mataifa matatu kwa pamoja ambayo ni Mexico, Marekani na Canada. Uwanja wa Estadio Azteca unaingia kwenye historia kwa kuwa moja ya viwanja vilivyowahi kutumika mara nyingi zaidi kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

Siku moja kabla ya mchezo wa ufunguzi, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Gianni Infantino, alizungumza na waandishi wa habari mjini Mexico City ambapo alijibu maswali mbalimbali kuhusu maandalizi ya mashindano hayo pamoja na changamoto zilizojitokeza kabla ya kuanza kwa michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.

Moja ya hoja zilizotawala mkutano huo ni malalamiko kuhusu bei kubwa za tiketi za mechi mbalimbali za Kombe la Dunia. Infantino alitetea mfumo wa upangaji wa bei hizo akisema kuwa hali hiyo si tofauti na matukio mengine makubwa ya michezo yanayofanyika Amerika Kaskazini.

“Watu wengi wanalalamika kuhusu bei za tiketi, lakini huu ndio mfumo unaotumika katika matukio mengi makubwa ya michezo hapa Amerika Kaskazini,” alisema Infantino.

Aidha, Infantino alizungumzia suala la mwamuzi wa Somalia, Omar Artan, ambaye ameripotiwa kushindwa kupata ruhusa ya kuingia Marekani. Kiongozi huyo wa FIFA alisema shirikisho hilo halikuwa na mamlaka ya kuingilia maamuzi ya serikali kuhusu utoaji wa vibali vya usafiri na uhamiaji.

Katika hatua nyingine, FIFA pia ilisifu ushirikiano uliowezesha timu ya taifa ya Iran kupata ruhusa ya kuingia Marekani kushiriki mashindano hayo licha ya changamoto za kidiplomasia zilizopo kati ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, mamia ya askari wa polisi wameonekana wakifanya doria katika maeneo mbalimbali ya Mexico City hususan katika uwanja wa ndege wa kimataifa na maeneo yanayozunguka uwanja wa Estadio Azteca. Hatua hiyo imekuja kufuatia hofu ya maandamano ya walimu pamoja na kuhakikisha usalama wa wageni na mashabiki wanaohudhuria ufunguzi wa michuano hiyo.

Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuwa moja ya mashindano makubwa zaidi kuwahi kufanyika, huku likishirikisha timu nyingi zaidi ukilinganisha na matoleo yaliyopita. Mashabiki duniani sasa wanasubiri kuona ni timu gani itaanza vizuri safari ya kusaka taji la dunia.

#Reply

#5Replies