Maneno ya Wema Sepetu baada ya kujifungua
Baada ya safari ndefu ya kusubiri kupata mtoto, staa wa filamu na mrembo wa Tanzania Wema Sepetu ameandika ujumbe wa hisia kali baada ya kujifungua mtoto wa kiume na kufungua ukurasa mpya katika maisha yake ya familia pamoja na mpenzi wake, Whozu.
Kupitia ujumbe wake uliosambaa mitandaoni, Wema alimshukuru Mungu kwa kile alichokiita muujiza wa maisha yao baada ya kipindi kirefu cha maombi na subira.
“Mungu ndiye Power, katupendelea… Yee kasema sawa, tulichongojea…” aliandika Wema kwa furaha kubwa.
Msanii huyo amesema hatua hiyo ni ushahidi kuwa Mungu hujibu maombi kwa wakati wake, hata pale ambapo watu wengi huanza kukata tamaa. Katika ujumbe wake, alimshukuru pia Whozu kwa kuwa sehemu ya safari hiyo muhimu ya maisha yao.
“Asante baba mtoto wangu… Mungu wetu ni mkali na ametujibu kwa wakati… Tuzidi kumtukuza na kumuabudu… Hakika tuliomba sana na ametushangaza…” ameongeza.
Mashabiki, watu maarufu pamoja na wadau wa burudani wameendelea kumpongeza Wema kwa hatua hiyo mpya ya kuwa mama, huku wengi wakisema simulizi yake imekuwa chanzo cha matumaini kwa wanawake wengi wanaopitia changamoto za kusubiri kupata mtoto.
Kwa muda mrefu, safari ya Wema kuhusu ndoto yake ya kuwa mama imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wake, jambo lililofanya taarifa ya kupata mtoto wake wa kwanza kugusa hisia za watu wengi ndani na nje ya Tanzania.
Mitandaoni, ujumbe wake umeendelea kusambazwa kwa kasi huku wengi wakieleza kuwa ni ushuhuda wa imani, subira na kutokata tamaa katika maisha.



Post a Comment