Marekani Kupunguza Vituo vya Uchakataji Visa Barani Afrika hadi 20

Serikali ya Marekani imetangaza mpango wa kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya balozi na ofisi za ubalozi (consulates) barani Afrika zinazoshughulikia maombi ya visa. Hatua hiyo itapunguza vituo vya uchakataji visa kutoka karibu vituo 50 vilivyopo sasa hadi vituo 20 pekee katika wiki zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa kutoka kwa maafisa wa Marekani na kumbukumbu ya ndani ya Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, uamuzi huo uliwasilishwa kwa wanadiplomasia wa Marekani, wakiwemo wakuu wa huduma za ubalozi, wakati wa mkutano wa simu uliofanyika Mei 29, 2026.

Inaelezwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliridhia mpango huo wiki iliyopita. Chini ya mfumo mpya, maombi mengi ya visa kutoka nchi mbalimbali za Afrika yataelekezwa katika vituo maalumu vilivyochaguliwa kuhudumia maeneo makubwa ya kikanda.

Miji iliyoorodheshwa kuwa vituo rasmi vya uchakataji visa ni pamoja na Abidjan (Côte d’Ivoire), Accra (Ghana), Addis Ababa (Ethiopia), Cape Town na Johannesburg (Afrika Kusini), Dakar (Senegal), Dar es Salaam (Tanzania), Djibouti (Djibouti), Kampala (Uganda), Kigali (Rwanda), Kinshasa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Lagos (Nigeria), Lomé (Togo), Luanda (Angola), Malabo (Equatorial Guinea), Monrovia (Liberia), Nairobi (Kenya), Port Louis (Mauritius), Praia (Cape Verde) na Yaoundé (Cameroon).

Ingawa tarehe rasmi ya kuanza kutekelezwa kwa mpango huo bado haijatangazwa, hatua hiyo inatarajiwa kubadili namna waombaji wa visa kutoka baadhi ya nchi za Afrika watakavyopata huduma za mahojiano na uchakataji wa nyaraka zao.

Wachambuzi wanaamini kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuongeza mzigo wa kazi katika vituo vilivyochaguliwa huku baadhi ya waombaji wakilazimika kusafiri umbali mrefu zaidi kufika kwenye vituo vya visa. Hata hivyo, uwepo wa Dar es Salaam katika orodha ya vituo vipya unamaanisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa miongoni mwa nchi zitakazotoa huduma za uchakataji visa za Marekani katika ukanda wake.

Mpango huu unakuja miezi kadhaa baada ya utawala wa Rais Donald Trump kuripotiwa kuwarejesha nyumbani mabalozi kutoka zaidi ya nchi 20 duniani, huku bara la Afrika likiwa miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko hayo ya kidiplomasia.

...See more

Reply

Discussions