Mwanamke Afariki Ndani ya Nyumba Yake, Polisi Wachunguza Kisa Kinachohusishwa na Utoaji Mimba
Maafisa wa upelelezi katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 35 ambaye alikutwa amefariki ndani ya nyumba yake akiwa pamoja na kijusi. Tukio hilo linachunguzwa kama kisa kinachoweza kuhusishwa na utoaji mimba usio salama.
Kwa mujibu wa polisi, tukio hilo liliripotiwa Mei 30 baada ya mpangaji mmoja kumjulisha mwenye nyumba kuwa mwanamke huyo alikuwa amelala sakafuni bila kuonyesha dalili zozote za uhai. Alionekana akiwa amezungukwa na damu nyingi ndani ya nyumba ambayo mlango wake ulikuwa wazi.
Polisi walifika eneo la tukio na kukuta mwili wa mwanamke huyo ukiwa ndani ya nyumba. Pia walikuta kijusi kilichokuwa bado kimeunganishwa na kondo la nyuma (placenta). Mwili huo ulihamishiwa katika Mochari ya Hospitali ya Kiambu Level 5 kwa ajili ya kuhifadhiwa wakati uchunguzi wa kitabibu ukiendelea kubaini chanzo halisi cha kifo.
Mamlaka zimesema uchunguzi unaendelea ili kufahamu mazingira yote yaliyosababisha tukio hilo. Wataalamu wa afya wamekuwa wakionya kuhusu ongezeko la matukio ya utoaji mimba usio salama, hali ambayo imeendelea kuhatarisha maisha ya wanawake katika maeneo mbalimbali.



Post a Comment