Parasite Yaongoza Orodha ya Filamu Bora za Karne ya 21
Filamu ya Korea Kusini, Parasite, imeibuka kileleni mwa orodha ya filamu 100 bora zaidi za karne ya 21, kulingana na tathmini mpya iliyotolewa na Rotten Tomatoes. Orodha hiyo inajumuisha filamu zilizotolewa kati ya mwaka 2000 na 2026 na imeandaliwa kwa kuzingatia maoni ya wakosoaji wa filamu pamoja na tathmini za watazamaji kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Filamu hiyo, iliyoongozwa na Bong Joon Ho, ilipata sifa kubwa kutokana na namna ilivyowasilisha tofauti za kiuchumi na kijamii kati ya familia mbili zenye maisha tofauti kabisa. Mafanikio yake yalizidi kuonekana baada ya kuandika historia kwa kushinda tuzo ya Oscar ya Filamu Bora, jambo lililoifanya kuwa filamu ya kwanza isiyo ya Kiingereza kufanikisha hatua hiyo.
Nafasi ya pili katika orodha hiyo imechukuliwa na Top Gun: Maverick, filamu iliyomrejesha nyota wa Hollywood Tom Cruise katika moja ya majukumu yake maarufu. Nafasi ya tatu imekwenda kwa Finding Nemo, ambayo bado inaendelea kupendwa na mashabiki wa filamu za uhuishaji licha ya kutolewa zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Miongoni mwa filamu zilizofanikiwa kuingia katika nafasi kumi za juu ni How to Train Your Dragon, Toy Story 3, Up, Godzilla Minus One, The Wrestler, Spotlight na A Separation.
Orodha hiyo pia imejumuisha filamu zilizovutia watazamaji duniani katika miaka ya hivi karibuni kama The Dark Knight, Avengers: Endgame, Oppenheimer, Spider-Man: Into the Spider-Verse na John Wick: Chapter 4.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tathmini hiyo, filamu zote zilizoorodheshwa zimeonyesha kiwango cha juu cha ubora kupitia mapokezi mazuri kutoka kwa wakosoaji na watazamaji. Vigezo vilivyotumika vilihusisha alama za ukosoaji, kura za mashabiki, idadi ya mapitio yaliyotolewa pamoja na umaarufu wa kila filamu katika soko la kimataifa.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa filamu za aina mbalimbali ikiwemo drama, uhuishaji, fantasy, horror na superhero zimeendelea kutawala tasnia ya filamu katika kipindi cha zaidi ya robo karne iliyopita, huku baadhi ya kazi zikiendelea kuwa na ushawishi mkubwa hata miaka mingi baada ya kutolewa kwake.



Post a Comment