Polisi Zanzibar Wafunga Uchunguzi wa Kifo cha Ashlee Robinson, Wasema Hakukuwa na Mauaji

Jeshi la Polisi Zanzibar limetangaza kukamilika kwa uchunguzi wa kifo cha raia wa Marekani na mwanaharakati wa mitandao ya kijamii, Ashlee Jenae Robinson, kilichozua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi yaliyotolewa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, ushahidi uliokusanywa unaonyesha kuwa Ashlee alipoteza maisha baada ya kujinyonga, huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni changamoto za msongo wa mawazo ambazo alikuwa akizikabili kwa muda.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea mwezi Aprili mwaka huu akiwa katika moja ya hoteli zilizopo Kaskazini mwa Unguja. Baada ya kuokotwa akiwa katika hali mbaya, alikimbizwa hospitalini kwa matibabu lakini baadaye alifariki dunia.

Wachunguzi walifanya mahojiano na watu mbalimbali waliokuwa karibu na marehemu pamoja na kuchambua taarifa za mawasiliano yake. Matokeo ya uchunguzi huo yalibaini kuwa kulikuwa na viashiria vya matatizo ya kisaikolojia na msongo wa mawazo kabla ya tukio hilo kutokea.

Kifo cha Ashlee kilisababisha mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu walidai huenda alihusika kuuawa na mchumba wake. Hata hivyo, polisi walieleza kuwa madai hayo yalichunguzwa kwa kina na hakuna ushahidi uliopatikana unaoonesha kuhusika kwa mtu mwingine katika kifo hicho.

Kutokana na hitimisho hilo, mamlaka zimeweka wazi kuwa uchunguzi umefungwa rasmi na matokeo yanaonesha kuwa tukio hilo halikuwa la mauaji bali lilihusishwa na hatua aliyochukua marehemu mwenyewe akiwa katika hali ya msongo wa mawazo.


Reply

Discussions