Trump Adai Iran Imeidungua Helikopta ya Kijeshi ya Marekani Katika Mlango wa Hormuz
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran imeidungua moja ya helikopta za kisasa za kijeshi za Marekani aina ya Apache wakati ikifanya doria katika eneo la Mlango wa Bahari wa Hormuz usiku wa kuamkia leo.
Kupitia taarifa yake, Trump alisema tukio hilo lilitokea wakati helikopta hiyo ikiwa kwenye operesheni ya kawaida ya ulinzi katika moja ya maeneo muhimu zaidi ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Hata hivyo, alieleza kuwa marubani wawili waliokuwa ndani ya helikopta hiyo walinusurika salama bila kupata majeraha yoyote licha ya shambulio hilo.
“Nimepata taarifa kutoka kwa jeshi letu kwamba usiku uliopita Iran iliidungua moja ya helikopta zetu za kisasa aina ya Apache wakati ikiwa kwenye doria katika eneo la Strait of Hormuz,” alisema Trump kupitia taarifa yake.
Tukio hilo limeongeza mvutano kati ya Marekani na Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, hasa kutokana na umuhimu wa Mlango wa Hormuz ambao hutumiwa na mataifa mengi kusafirisha mafuta kupitia bahari.
Mpaka sasa, mamlaka za Iran hazijatoa taarifa rasmi kuhusu madai hayo, huku wachambuzi wa siasa za kimataifa wakisema tukio hilo linaweza kuongeza taharuki ya kiusalama katika ukanda huo.
Jeshi la Marekani pia linaendelea kufanya tathmini ya tukio hilo pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya shambulio hilo kuripotiwa.


Post a Comment