Wanafunzi Nane Wakamatwa Kufuatia Moto wa Shule Ulioua Wanafunzi 16 Nchini Kenya
Mamlaka za usalama nchini Kenya zimewakamata wanafunzi wanane wa shule ya wasichana ya Utumishi Girls Academy baada ya kuhusishwa na tukio la moto lililosababisha vifo vya wanafunzi 16.
Moto huo ulitokea alfajiri ya Alhamisi katika shule hiyo iliyopo Gilgil, takribani kilomita 120 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Nairobi. Moto huo uliteketeza sehemu ya juu ya bweni lililokuwa na vitanda vya ghorofa 135, na kusababisha maafa makubwa kwa wanafunzi waliokuwa wakilala.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi la Kenya, uchunguzi uliohusisha mahojiano na wanafunzi pamoja na wafanyakazi wa shule, sambamba na uchambuzi wa picha za kamera za usalama (CCTV), uliwawezesha wachunguzi kubaini wanafunzi wanane kama watu wanaohusishwa na mipango na utekelezaji wa tukio hilo.
Polisi walieleza kuwa baadhi ya wanafunzi hao walifuatiliwa hadi majumbani mwao na kurejeshwa shuleni kwa ajili ya kuhojiwa, huku wengine waliokuwa bado katika eneo la Gilgil wakikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Hadi sasa, chanzo halisi cha moto huo bado hakijabainika rasmi, na uchunguzi unaendelea. Mamlaka zimeahidi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira yote yaliyosababisha janga hilo.
Tukio hilo limeibua huzuni kubwa nchini Kenya, huku familia za wanafunzi, viongozi wa elimu na wananchi wakitaka ukweli wote ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika watakaobainika.
Moto wa shule umekuwa changamoto inayojirudia nchini Kenya katika miaka ya nyuma, ambapo baadhi ya matukio yamehusishwa na migogoro ya wanafunzi, utovu wa nidhamu au mapungufu katika mifumo ya usalama wa shule. Wataalamu wa elimu wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama wa mabweni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wanafunzi kuhusu madhara ya vitendo vya uharibifu.


Post a Comment