Watu watano wafariki katika ajali ya treni ya Warri–Itakpe nchini Nigeria
Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia ajali ya treni kwenye reli ya Warri–Itakpe nchini Nigeria imeongezeka hadi watu watano, wakiwemo watu wazima wanne pamoja na mtoto mchanga mmoja.
Ajali hiyo ilitokea Jumatatu, Juni 8, 2026 karibu na eneo la Agbor katika Jimbo la Delta, wakati treni ya huduma ya Warri–Itakpe Train Service (WITS) ilipopata hitilafu na baadhi ya mabehewa kuacha njia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uchukuzi ya Nigeria pamoja na Shirika la Reli nchini humo (NRC), mabehewa manne yalipinduka huku behewa moja likitoka kabisa kwenye reli, hali iliyosababisha vifo hivyo pamoja na majeruhi wengi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa watu 24 walijeruhiwa vibaya, huku wengine kadhaa wakipata majeraha ya viwango tofauti na kuendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Wakati ajali hiyo ikitokea, jumla ya watu 482 walikuwa ndani ya treni hiyo, wakiwemo abiria 442 pamoja na wafanyakazi, maafisa wa usalama na watoa huduma wengine 40.
Operesheni za uokoaji zilianza mara moja kwa ushirikiano wa Serikali ya Jimbo la Delta, mamlaka ya dharura ya NEMA, kikosi cha usalama barabarani FRSC, Polisi, Civil Defence pamoja na viongozi wa eneo hilo.
Miongoni mwa waliohusika kusaidia shughuli za uokoaji ni Seneta wa Delta Central, Seneta Dafinone, pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Serikali ya Jimbo la Delta, Patrick Ukah.
Aidha, mfanyakazi mmoja wa Shirika la Reli la Nigeria anaripotiwa kupata jeraha kubwa kwenye kiungo cha mwili lakini hali yake imeelezwa kuwa imetulia huku akiendelea na matibabu.
Mamlaka nchini Nigeria zimeanza uchunguzi wa kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo huku juhudi za kuwahudumia majeruhi na familia za waathirika zikiendelea.


Post a Comment