WHO Yaonya,Hofu na Imani Potofu Vinakwamisha Mapambano Dhidi ya Ebola DRC

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kuwa upinzani kutoka kwa baadhi ya jamii nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unaendelea kuwa changamoto kubwa katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, huku wahudumu wa afya wakikabiliwa na mazingira hatarishi wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa Dharura wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Marie-Rosaline Belizaire, amesema tukio la hivi karibuni limeonesha namna kutokuaminiana kwa wananchi kunavyoweza kuhatarisha afya ya jamii nzima.

Kwa mujibu wa Dkt. Belizaire, timu ya wataalamu wa afya ilifika kusaidia familia iliyopoteza ndugu kutokana na Ebola ili kuhakikisha mazishi yanafanyika kwa usalama na kwa kuzingatia heshima. Hata hivyo, baadhi ya wanafamilia walikataa kuamini matokeo ya vipimo na kuonesha upinzani dhidi ya wahudumu hao.

Hali ilizidi kuwa ngumu baada ya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kutoa vitisho vya kuwaita watu wenye silaha, jambo lililolazimisha timu ya afya kuondoka kwa haraka kwa sababu za kiusalama. Baada ya kuondoka kwao, mwili wa marehemu ulisafirishwa na wanajamii bila kufuata taratibu za afya, hatua iliyoongeza hatari ya maambukizi mapya.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa hadi Juni 3, DRC ilikuwa imethibitisha wagonjwa 381 wa Ebola huku watu 64 wakipoteza maisha. Nchini Uganda, wagonjwa 15 walikuwa wamethibitishwa kuugua ugonjwa huo na kifo kimoja cha mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola kiliripotiwa.

WHO imebainisha kuwa licha ya mafanikio makubwa katika kuongeza uwezo wa upimaji wa Ebola kutoka vipimo 40 kwa siku mwanzoni mwa mlipuko hadi zaidi ya vipimo 800 kwa siku sasa, changamoto ya kuaminika kwa taarifa za afya bado ipo.

Dkt. Belizaire amesema sababu kuu za hali hiyo ni pamoja na imani za kitamaduni, taarifa zisizo sahihi pamoja na kufanana kwa dalili za Ebola na magonjwa mengine ya kawaida kama malaria. Katika baadhi ya maeneo, wananchi bado huamini kuwa vifo na magonjwa husababishwa na uchawi au sumu badala ya maambukizi ya virusi.

Amesisitiza kuwa juhudi za WHO na wadau wa afya hazilengi kupinga au kubadilisha tamaduni za wananchi, bali zinakusudia kuunganisha elimu ya kisayansi na mifumo ya kijamii ili kuongeza uelewa na ushirikiano katika mapambano dhidi ya Ebola. Kwa mujibu wake, ushirikiano wa jamii ndiyo silaha muhimu zaidi katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari.

Reply

Discussions