Showing posts with label Jukwaa la Familia. Show all posts
Showing posts with label Jukwaa la Familia. Show all posts

Umemuandaaje mwanao kuwa mtu boraAfyaclass Forum •

Tumetumia muda mwingi  kumfundisha mtoto wa kike na kusahau kuwa hiki kichwa (mume) kinatakiwa kufunzwa ili kifananie na  Kristo kwa maana nyingine tabia za Kimungu zionekane ndani ya mwanaume.



Bwana Yesu apewe sifa, karibu katika tafakari ya ujumbe wa leo. Mimi ninayekuletea ujumbe huu ni mtumishi wa Mungu Mwalimu Peace Marino  kutoka KKKT Usharika wa Ebeneza Nyashimo Jimbo la Kaskazini Busega.

Kipindi hiki watoto wamefunga shule na wapo nyumbani kwa ajili ya likizo ya masomo. Hiyo ni nafasi ya kipekee wazazi kukaa na watoto na kuwajenga katika msingi wa maadili yanayompasa ikiwamo kumfundisha kusali, kufanya maombi na kumcha Mungu kwa ujumla. Watoto wengi hupendelea kusafiri kwenda maeneo mbalimbali pamoja kutembelea ndugu jamaa na marafiki.

Licha ya hayo yote, Ujumbe tuliopewa leo ninataka kuzungumza nawe mzazi juu ya hatima bora ya vijana wetu wa kiume. Somo letu limebeba ujumbe “Umemuandaaje mwanao wa kiume kuwa mtu bora?”

Jamii nyingi zimekuwa zikimthamini mtoto wa kiume na kumpa hadhi kubwa na kusahau kuwa anahitaji mafunzo yatakayomsaidia kuwa bora katika jamii, kwenye kanisa na Taifa kwa ujumla.

Efeso 5:23b inasema "Kwa Maana mume ni kichwa cha mkewe kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa.”

Tumetumia muda mwingi  kumfundisha mtoto wa kike na kusahau kuwa hiki kichwa (mume) kinatakiwa kufunzwa ili kifananie na  Kristo kwa maana nyingine tabia za Kimungu zionekane ndani ya mwanaume.

Tito 2:3-4. Inazungumza kwa habari ya wazee wa kike kufundisha mema na kuwapa maarifa wanawake, vijana ikiwa ni pamoja na kuwa na kiasi, kuwa safi, kufanya kazi, kuwa wema, kuwatii waume zao, kuwa wavumilivu na mambo mengine mengi. Jamii na kanisa tumejitahidi sana kutimiza jukumu hili.

Watoto wa kike wanapokosea tunawawajibisha kwelikweli na hakuna mama au baba anayetaka binti yake aharibikiwe, hivyo jicho la baba na mama liko kwa mtoto wa kike. Wakati mwingine hatujawapa nafasi ya kujieleza kwa nini amekosa au ameingia kwenye changamoto fulani badala yake huwa tunawaadhibu bila hata kujua chanzo cha tatizo. Tunafanya yote haya kwa sababu ya kuogopa kupata aibu.

Naomba nikuulize mpendwa, hivi nguvu unayotumia kumlinda binti yako ni sawa na unayotumia kumlinda mwanao wa kiume? Kwa nini? Binti akichelewa kurudi nyumbani anaadhibiwa vikali lakini kijana wa kiume hata aingie usiku jamii inaona ni sawa tu, jambo kama hili siyo sawa kwani halimuandai mwanao wa kiume kuwa bora.

Tito:2:6. Inasema “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi.” Katika hili tunahitaji rehema ya Mungu kwani tumesahau kabisa kuwa tunalo jukumu la kuwasaidia watoto wa kiume na kama tunafanya ni kwa kiasi kidogo sana. Hatuna budi sasa kuamka na kulichukulia jambo hili kwa uzito ili kunusuru kizazi chetu.

Paulo anamwambia Timotheo 1:5 kuwa, “Naikumbuka imani uliyonayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisina katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo”

 “Kina mama hawa walimfundisha kijana wao na kumrithisha imani akakua nayo na hakuiacha. Wewe unawarithisha nini wanao, nani anajivunia wanao kutokana na jinsi ulivyowafunza vizuri?

Tupate wapi kina baba kama Ayubu tusipowafundisha? Tupate wapi kinababa ambao Mungu anajivunia tusipowafundisha? (Ayubu1:5) Ayubu aliamka asubuhi na mapema akasogeza sadaka kwa hesabu ya watoto wake wote akisema yamkini hawa wanangu wamefanya dhambi na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Tunao kina baba wangapi katika jamii zetu wanaokumbuka kutoa sadaka kwa ajili ya watoto wao au hata kufunga na kuomba kwa ajili ya watoto wao na uzao wao?

Kila binti anatamani kuolewa na kijana mwenye hofu ya Mungu ndani yake. Hiyo hofu ya Mungu atatolea wapi ikiwa hakuna wa kumfundisha? Wazazi tumekataa wachumba ambao mabinti zetu wametuletea kwa sababu tuliwaona hawana hofu ya Mungu ndani yao, kama hujaweza kumfundisha mwanao wa kiume ili afae kuwa mume wa binti fulani kina nani watamfundisha mkweo?

Binti akibeba mimba nje ya utaratibu ni kosa lisilo sameheka, mama itabidi utoe maelezo ya kutosha kwa baba yake limetokeaje jambo hilo. Mabinti wengine wamepigwa, wengine wamefukuzwa na maisha yao yakaharibika kabisa, lakini vipi kama kilichompata ni kama kile kilichompata Dina (Mwanzo 34) na Tamari (2 Samweli 13:1-14) mabinti hawa walibakwa. Wakati mwingine mabinti zetu wanapitia changamoto nyingi na ngumu na hawana namna na wapi pa kusemea. Ni lini baba au mama umekaa na binti yako na kutaka kujua anapitia changamoto gani?

Jambo kama hili linapotokea kwa watoto wa kiume hatuoni kama lina madhara linachukuliwa kama jambo la kawaida. Mwanzo 34:8 Shekemu anapomtendea hiana Dina, baba yake Shekemu (Hamori) anakwenda kwa Yakobo kuomba watoto waoane bila hata kujali ni maumivu kiasi gani Dina anapitia. Hatuoni ni wapi Hamori anamuwajibisha mwanaye wa kiume kwa kosa alilolifanya. Mpendwa dhambi yoyote anayoifanya mwanao wa kiume na ukaifumbia macho ni mbegu unapanda na matunda yake utayaona, Yesu atuhurumie.

Tunapohitimisha nikusihi, umwangalie mwanao wa kiume kwa ukaribu na kumfundisha kama unavyofanya kwa mwanao wa kike ili kila mmoja afae kwa ufalme wa Mungu. Mungu akubariki sana.

Mhubiri ni Mwalimu Peace Marino kutoka KKKT Usharika wa Ebeneza Nyashimo, Jimbo la Kaskazini Busega mkoani Simiyu.

0 Comment

Familia imefikia makubaliano na serikali juu ya mazishi ya Raisi Edgar Lungu Afyaclass Forum •

Familia imefikia makubaliano na serikali juu ya mazishi ya Raisi Edgar Lungu 



Baada ya tamko la Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu ambalo yalikuwa ni maagizo yake ya kwamba mpinzani wake wa kisiasa na Rais wa sasa Hakainde Hichilema hapaswi kufika popote karibu na mwili wake familia imefikia makubaliano na serikali juu ya mazishi ya Kiongozi Huyo na mpango wa mazishi umekamilika.

Baada ya Mazungumzo ya muda mrefu baina ya familia ya Lungu wamekubaliana kwamba Mwili wa Rais huyo wa zamani utasafirishwa kutoka Afrika Kusini kwenda mji mkuu wa Zambia, Lusaka siku ya Jumatano wiki hiii kwa ndege binafsi ya kukodi, na baada ya kuwasili utapokelewa na familia na kisha kutakuwa na heshima kamili ya Kijeshi na baada ya hapo utasafirishwa kwenda kwenye makzi yake mjini Lusaka. 

Aidha wananchi wa Zambia watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwanzia alhamis na zoezi hilo litakamilika siku ya jumamosi ambapo Mazishi ya Kitaifa yatafanyika jumapili Juni 22, 2025 na maombolezo yatakamilika jumatatu ambapo mapaka sasa bado haijajulikana endapo atazikwa katika eneo rasmi la mazishi ya Rais au katika makazi yake binafsi.

Hata hivyo msemaji wa familia Makebi Zulu katika mazungumzo yake na vyombo vya habari akiwa pamoja na Katibu wa Baraza la Mawaziri la Zambia Patrick Kangwa amesema familia hiyo imeomba radhi kwa usumbufu na maumivu ambayo mazungumzo ya muda mrefu yamesababisha ambapo amesema wamefanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaheshimu matakwa ya kibinafsi ya Rais wa zamani.

Sambamba na hilo kwa upande wa serikali Katibu Mkuu wa serikali Patrick Kangwa amewashukuru wananchi wa Zambia kwa uvumilivu wao wakati huu mgumu ambapo kwa upande wa familia umesisitiza kuwa wanaamini kuwa Serikali haitakwenda kinyume na makubaliano yao.

0 Comment

Mbinu bora za kumlea Mtoto wako katika njia SahihiAfyaclass Forum •

Mbinu bora za kumlea Mtoto wako katika njia Sahihi



Katika safari ya maisha ya mtoto, makuzi ni hatua nyeti inayojengwa kwa msingi wa maadili, malezi na mazingira yanayomzunguka.

Watoto wanapokua, hukutana na changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni ushawishi kutoka kwa marafiki au makundi ya wenzao.

Baadhi ya makundi haya huwapeleka kwenye njia potofu kama vile wizi, matumizi ya dawa za kulevya, uasherati, au tabia zisizokubalika na jamii.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa watoto kujifunza jinsi ya kuchagua marafiki kwa busara na kuepuka kushawishiwa kufanya maovu.

Wakati huohuo, wazazi pia wanayo nafasi kubwa sana ya kuhakikisha watoto wao wanabaki kwenye msingi wa maadili sahihi.

Wapo baadhi ya watu wanaweza kujiuliza, mtoto mdogo mfano mwenye miaka 6 au saba, anawezaje kuepuka haya kutoka kwa wenzake wenye ushawishi.
wataalamu wa saikolojia wanasema, watoto wanapaswa kufundishwa kujitambua wangali na umri mdogo.

Hiyo itmsaidia kuelewa maadili wanayoamini na kujua mambo wanayopaswa kuyakataa. Kwa sababu ile hali ya kujitambua, mara zote huwasaidia kuwa na msimamo katika kila uamuzi anaotaka kuufanya.

Pia hata kama atakumbana na shinikizo kutoka kwa marafiki, mtoto akiwa na misingi thabiti ya maadili, siyo rahisi kushawishika.

Kwa maana nyingine, watoto wanapofundishwa namna ya kuchagua marafiki waadilifu, huwa na uwezekano mdogo wa kujiingiza katika makundi mabaya.

Marafiki wenye hofu ya Mungu, wenye maadili na wanaojali masomo au shughuli halali huwa na ushawishi chanya.

Hivyo wazazi na walimu wanapaswa kuwasaidia kutambua tofauti kati ya marafiki wanaojenga na wanaoharibu.
lakini pia siyo kila ombi au shauri linastahili kukubaliwa. Ni vema watoto wafundishwe namna ya kusema “hapana” kwa ujasiri, wanapokabiliwa na shinikizo la wenzao.

Tukumbuke, elimu ya kujiepusha na vishawishi viovu ni silaha madhubuti kwa mtoto.

Kitu kingine kinachoweza kumsaidia mtoto kuenenda katika njia sahihi ni kwa mzazi kumuhimiza mwanao ashiriki michezo, vikundi vya dini, sanaa, au shughuli za shule.

Njia hii nayo huwasaidia watoto wengi kuwa na ratiba yenye maana na kujiepusha na makundi yenye mienendo mibaya na mazingira haya pia huwapa nafasi ya kujenga mitazamo mizuri na kupata marafiki bora.

Mara zote, watoto wanaojua wanachotaka maishani, huwa waangalifu kuhusu mwenendo wao na marafiki wanaowazunguka.

Malengo hutoa dira ya maisha na kumzuia mtoto asiingie kwenye makundi yatakayoharibu ndoto zake. Lakini ili haya yafanikiwe, tukumbuke kuwa watoto hujifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi.
na wengi wao hujifunza zaidi kwa kuangalia kuliko kusikia. Wazazi wanapaswa kuishi kwa maadili mema kama kusema ukweli, kuheshimu wengine na kushughulikia matatizo kwa njia ya amani.

Ni wazi kuwa watoto wanaopata mfano mzuri nyumbani, huwa na uwezekano mkubwa wa kufuata maadili.

Wazazi wanapaswa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara kuhusu changamoto wanazokutana nazo, marafiki zao na mazingira yao ya kila siku.

Mawasiliano haya hujenga uaminifu na kumwezesha mtoto kujisikia huru kueleza matatizo au mashaka anayokumbana nayo.
Watoto wanahitaji mipaka inayoeleweka kuhusu nini wanaruhusiwa na kipi hapana. Nidhamu siyo adhabu tu, bali pia ni njia ya kuwaelekeza kwenye mwelekeo sahihi. Nidhamu inayotolewa kwa upendo hujenga heshima na uwajibikaji.

Hivyo watoto wenye imani ya ndani wanaweza kufanya uamuzi sahihi bila kuathiriwa na makundi mabaya.

Ni wakati wa wazazi kuendelea kuwahimiza na kuwapongeza wanapofanya vizuri na kuwasaidia kujifunza kutokana na makosa.

Malezi si jukumu la mzazi pekee. Wazazi wanapaswa kushirikiana na walimu, viongozi wa dini na wanajamii wengine kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua kimaadili.

Tukubali tusikubali, watoto pia wanao uwezo wa kufanya uamuzi mzuri endapo watapata mwongozo sahihi kutoka kwa wazazi na walezi wao.

Ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha watoto wanalelewa kwa msingi wa maadili mema, wanaongozwa kuepuka makundi mabaya na wanajengewaa mazingira yatakayowawezesha kuwa raia wema wa sasa na baadaye.

Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunalinda kizazi cha sasa na kuandaa Taifa bora la miaka ijayo.

0 Comment
Notification
Karibu Afyaclass Forum Jukwaa linalojadili mambo mbali mbali ikiwemo afya,Magonjwa na Updates Zote,Tembelea hapa kila Siku,Pia Share Maoni yako kwenye jukwaa hili Afyaclass Forum ASANTE.
UNDERSTOOD