Mbinu bora za kumlea Mtoto wako katika njia Sahihi
Katika safari ya maisha ya mtoto, makuzi ni hatua nyeti inayojengwa kwa msingi wa maadili, malezi na mazingira yanayomzunguka.
Watoto wanapokua, hukutana na changamoto mbalimbali, mojawapo ikiwa ni ushawishi kutoka kwa marafiki au makundi ya wenzao.
Baadhi ya makundi haya huwapeleka kwenye njia potofu kama vile wizi, matumizi ya dawa za kulevya, uasherati, au tabia zisizokubalika na jamii.
Kwa hiyo, ni muhimu kwa watoto kujifunza jinsi ya kuchagua marafiki kwa busara na kuepuka kushawishiwa kufanya maovu.
Wakati huohuo, wazazi pia wanayo nafasi kubwa sana ya kuhakikisha watoto wao wanabaki kwenye msingi wa maadili sahihi.
Wapo baadhi ya watu wanaweza kujiuliza, mtoto mdogo mfano mwenye miaka 6 au saba, anawezaje kuepuka haya kutoka kwa wenzake wenye ushawishi.
wataalamu wa saikolojia wanasema, watoto wanapaswa kufundishwa kujitambua wangali na umri mdogo.
Hiyo itmsaidia kuelewa maadili wanayoamini na kujua mambo wanayopaswa kuyakataa. Kwa sababu ile hali ya kujitambua, mara zote huwasaidia kuwa na msimamo katika kila uamuzi anaotaka kuufanya.
Pia hata kama atakumbana na shinikizo kutoka kwa marafiki, mtoto akiwa na misingi thabiti ya maadili, siyo rahisi kushawishika.
Kwa maana nyingine, watoto wanapofundishwa namna ya kuchagua marafiki waadilifu, huwa na uwezekano mdogo wa kujiingiza katika makundi mabaya.
Marafiki wenye hofu ya Mungu, wenye maadili na wanaojali masomo au shughuli halali huwa na ushawishi chanya.
Hivyo wazazi na walimu wanapaswa kuwasaidia kutambua tofauti kati ya marafiki wanaojenga na wanaoharibu.
lakini pia siyo kila ombi au shauri linastahili kukubaliwa. Ni vema watoto wafundishwe namna ya kusema “hapana” kwa ujasiri, wanapokabiliwa na shinikizo la wenzao.
Tukumbuke, elimu ya kujiepusha na vishawishi viovu ni silaha madhubuti kwa mtoto.
Kitu kingine kinachoweza kumsaidia mtoto kuenenda katika njia sahihi ni kwa mzazi kumuhimiza mwanao ashiriki michezo, vikundi vya dini, sanaa, au shughuli za shule.
Njia hii nayo huwasaidia watoto wengi kuwa na ratiba yenye maana na kujiepusha na makundi yenye mienendo mibaya na mazingira haya pia huwapa nafasi ya kujenga mitazamo mizuri na kupata marafiki bora.
Mara zote, watoto wanaojua wanachotaka maishani, huwa waangalifu kuhusu mwenendo wao na marafiki wanaowazunguka.
Malengo hutoa dira ya maisha na kumzuia mtoto asiingie kwenye makundi yatakayoharibu ndoto zake. Lakini ili haya yafanikiwe, tukumbuke kuwa watoto hujifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi.
na wengi wao hujifunza zaidi kwa kuangalia kuliko kusikia. Wazazi wanapaswa kuishi kwa maadili mema kama kusema ukweli, kuheshimu wengine na kushughulikia matatizo kwa njia ya amani.
Ni wazi kuwa watoto wanaopata mfano mzuri nyumbani, huwa na uwezekano mkubwa wa kufuata maadili.
Wazazi wanapaswa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara kuhusu changamoto wanazokutana nazo, marafiki zao na mazingira yao ya kila siku.
Mawasiliano haya hujenga uaminifu na kumwezesha mtoto kujisikia huru kueleza matatizo au mashaka anayokumbana nayo.
Watoto wanahitaji mipaka inayoeleweka kuhusu nini wanaruhusiwa na kipi hapana. Nidhamu siyo adhabu tu, bali pia ni njia ya kuwaelekeza kwenye mwelekeo sahihi. Nidhamu inayotolewa kwa upendo hujenga heshima na uwajibikaji.
Hivyo watoto wenye imani ya ndani wanaweza kufanya uamuzi sahihi bila kuathiriwa na makundi mabaya.
Ni wakati wa wazazi kuendelea kuwahimiza na kuwapongeza wanapofanya vizuri na kuwasaidia kujifunza kutokana na makosa.
Malezi si jukumu la mzazi pekee. Wazazi wanapaswa kushirikiana na walimu, viongozi wa dini na wanajamii wengine kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua kimaadili.
Tukubali tusikubali, watoto pia wanao uwezo wa kufanya uamuzi mzuri endapo watapata mwongozo sahihi kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha watoto wanalelewa kwa msingi wa maadili mema, wanaongozwa kuepuka makundi mabaya na wanajengewaa mazingira yatakayowawezesha kuwa raia wema wa sasa na baadaye.
Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunalinda kizazi cha sasa na kuandaa Taifa bora la miaka ijayo.
REPLY HAPA
image quote pre code