Ticker

6/recent/ticker-posts

Tatizo la Afya ya Akili na Ugonjwa wa Sonona



Tatizo la Afya ya Akili na Ugonjwa wa Sonona
whatsapp sharing button
Afya ya Akili

Afya ya akili maana yake ni hali ya kuwa sawa kihisia, kisaikolojia na kijamii inayoambatana na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za kila siku. Ni hali ya kuwa na mawazo chanya, kuwa sawa kijamii na kisaikolojia na kuweza kuchangia katika utendaji wako na uwezo wa kuridhisha wa kimawazo na kitabia. Huhusisha uwezo wa mtu kumudu mfadhaiko wa kihisia kama vile wasiwasi, upweke, hasira, huzuni; ikiwa na maana ya kuwa mstahimilivu na kuwa na mchango katika jamii inayomzunguka.

Afya ya akili inaathiri jinsi tunavyofikiri, kuhisi, na kutenda. Pia husaidia kuamua jinsi tunavyokabiliana na mafadhaiko, kuhusiana na wengine, na kufanya maamuzi yanayofaa. Afya ya akili ni muhimu katika kila hatua ya maisha, kuanzia utotoni na ujana hadi utu uzima. Kumekuwa na tafsiri ambayo si sahihi katika jamii yetu ya kuwa afya ya akili ni hali ya kutokuwa sawa, afya ya akili ni tatizo, afya ya akili ni ugonjwa wa akili, afya ya akili ni upungufu wa akili. Tafsiri hizi zote hazipo sawa. Ukweli ni kwamba afya ya akili ni afya; hakuna afya pasipo afya ya akili. Afya ya akili sio ugonjwa wa akili na hakuna kitu kinachoitwa ugonjwa wa afya ya akili. Kuna umuhimu wa kujifunza maneno haya ili kupunguza unyanyapaa wa afya ya akili katika jamii zetu.

Ugonjwa wa Akili

Ugonjwa wa akili ni hali ya kutokuwa sawa inayoathiri utendaji kazi wa mtu na madiliko huweza kuonekana katika hisia, fikra na matendo tofauti na yale yanayotarajiwa na jamii na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha. Kuna zaidi ya magonjwa 200 ya akili, ikiwa ni pamoja na sonona, uraibu, wasiwasi uliopitiliza, skizofrenia, baipolar (mawazo mseto).

Ugonjwa wa Sonona

Sonona ni ugonjwa wa akili unaohusisha hali endelevu ya huzuni au kukosa shauku au raha inayoambatana na mabadiliko mbalimbali ya kimwili, kihisia na kiakili pia. Sonona ni hali inayoathiri utendaji kazi mzima wa mtu. Kuna utofauti mkubwa kati ya sonona na msongo wa mawazo. Aidha, msongo wa mawazo uliokithiri huweza kusababisha sonona.

Ugonjwa huu unatokana na namna tunavyotatua changamoto tunazokutana nazo katika maisha yetu ya kila siku. Sonona ni mrejesho wa hisia tulizozibeba ndani yetu kutokana na nyakati mbalimbali tunazozipitia. Hii inaweza kuwa kwa kupanga kutokana na utofauti katika utatuzi wa changamoto zetu. Kushindwa kukabiliana na changamoto za maisha ndio mwanzo wa kupata sonona. Sonona ni moja kati ya magonjwa ya afya ya akili ulimwenguni ikiwa na zaidi ya watu milioni 264 kwa mwaka wanaoathirika na changamoto hii. Hii ni hali inayoongoza kwa kuleta mzigo mkubwa kwa wagonjwa wengi duniani na katika hali iliyokithiri inaweza kusababisha mtu kuondoa uhai wake.

Watu wengi hupata msongo wa mawazo, ikiwa ni changamoto ya afya ya akili na ni hali ya kawaida kukutana nayo katika maisha. Msongo wa mawazo ukikithiri hupelekea sonona. Sonona pia ikikithiri hupelekea tatizo liitwalo Sonona Kubwa (Major Depressive Disorder, MDD). Sonona Kubwa ni kiwango cha juu cha tatizo ambacho kinahitaji matibabu ya haraka na kitaalamu zaidi.

Takwimu zinaonesha kuwa takriban watu milioni 350 wameathirika na magonjwa ya akili na zaidi ya watu 800,000 kila mwaka hufariki kwa kuondoa uhai wao wenyewe na hii hutokea sana kwa vijana kuanzia umri wa miaka 15 hadi 29. Ongezeko la changamoto za afya ya akili linakuja kwa kasi ulimwenguni kote ikiwemo Tanzania.

Kutokana na malengo ya maendeleo endelevu (SDG) yaliyooanzishwa mwaka 2015 na Baraza la Umoja wa Mataifa likiwa na malengo ya kufikiwa mwaka 2030, mkusanyiko huo wa malengo 17 yaliyopangiliwa kwa faida ya watu wote; lengo namba tatu ambalo ni “Afya Njema na Ustawi” linahakikisha kila mtu anapata huduma za afya bora. Sonona ni moja kati ya vipaumbele vya Shirika la Afya Duniani kupitia mpango mkakati uitwao WHO’s Mental Health Gap Action Programme (mhGAP) ikilenga kusaidia nchi mbalimbali, haswa kwa nchi za kipato cha chini na kati kuongeza utoaji huduma juu ya afya ya akili na magonjwa mbalimbali ya mfumo wa fahamu.

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na Lancet Global Health, zinaonesha kuwa kuna uhaba wa takwimu juu ya afya ya akili barani Afrika hali ambayo inaonesha ni jinsi gani bado huduma hizi ni duni barani. Changamoto za afya ya akili zimekuwa zikiongezeka kwa kiasi kikubwa barani Afrika, kitu ambacho kinahitaji kuwekewa mkazo wa hali ya juu. Idadi ya watu barani Afrika inasadikika kuongezeka mara mbili katika miongo mitatu ijayo. Ongezeko la watu linaenda sambamba na ongezeko la changamoto za afya ya akili. Watu wengi hasa vijana wako katika hatari ya kuathirika na changamoto hizi, hii ikitokana na misukumo mbalimbali katika jamii na utumiaji wa dawa za kulevya ukiongezeka ikiwa kama njia kuu ya wahanga hawa kutumia kuepukana na changamoto hizo.

Je, Utajuaje Kama Una Sonona?

Ubaya ni pale ambapo mgonjwa wa sonona hajijui kama anasonona. Hii inapelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya waathirika na kukithiri kwa tatizo. Sonona ni ugonjwa usiofichika. Kupitia muongozo wa magonjwa mbalimbali ya akili (DSM V) pamoja na toleo la Kiswahili – Tiba Baina ya Watu (TBW) kwa International Rescue Committee (IRC) kutoka kwa Shirika la Afya Duniani tunaweza kuona vitu mbalimbali vinavyoweza kuashiria kuwa wewe ni muathirika wa ugonjwa wa akili, sonona. Dalili za sonona hujumuisha:

  • Mabadiliko ya usingizi aidha kulala sana ama kukosa usingizi kabisa.
  • Mabadiliko katika kula, aidha kukosa kabisa hamu ya kula ama kula sana.
  • Hisia za kujiona mwenye hatia au hufai.
  • Hisia za uchovu na umakini hafifu kazini.
  • Kukosa utulivu wa mwili na kihisia pia.
  • Ugumu katika kufanya maamuzi.
  • Kupungua uzito bila kutarajia, takribani 5% kwa mwezi ama kuongezeka uzito.
  • Kusononeka kila wakati, huzuni endelevu.
  • Kujitenga mbali na watu na kupendelea kukaa peke yako muda mwingi.
  • Kukosa matumaini kabisa.
  • Kupoteza msisimko wa kihisia na kukosa hamu ya tendo la ndoa.
  • Kuwa mvivu hata kwenye shughuli za kawaida.
  • Kupata maumivu ya mwili kama vile kichwa kuuma mara kwa mara, vidonda vya tumbo, kujihisi mchovu mara kwa mara, kushindwa kuzungumza, kushindwa kutembea.
  • Kuwa na hasira mara kwa mara hata sehemu zinazohitaji utulivu.
  • Kujawa na chuki juu ya wengine na kutoelewana na watu wanakuzunguka.
  • Kutamani kujidhuru na hatimaye kuondoa uhai wa mtu binafsi au pamoja na wale wanaomtegemea.
  • ubadilika katika siku za hedhi au kukosa kabisa.
  • Uraibu hasa wa pombe.
  • Kusahau na kukosa uwezo wa kufikiri vema.

Sababu za Ugonjwa wa Sonona

Visababishi vya ugonjwa wa sonona vinaweza kuwa katika makundi makuu matatu: kibailojia, kisaikolojia na kijamii.

1. Sababu za Kibailojia

  • Kurithi kwa vinasaba vya ugonjwa wa sonona. Uwepo wa historia ya ugonjwa huu katika familia huongeza uwezekano wa mtu kupata tatizo hili. Hii inamaanisha ugonjwa huu unaweza ukawa ni wa kurithi kutoka kizazi hadi kizazi, japokuwa kutokuwepo kwa historia ya ugonjwa huu katika familia haina maana ya kuwa hakuna uwezekano wa kupata.
  • Magonjwa ya mwili. Magonjwa ya mwili aidha ya muda mfupi kama vile malaria kali ama magonjwa sugu yaani ya muda mrefu kama vile kisukari, homa ya ini, saratani, UKIMWI, figo kushindwa kufanya kazi, nk.

2. Sababu za Kisaikolojia

  • Malezi. Watu wengi wanaopata ugonjwa huu wa sonona huwa wanahistoria ya kupata changamoto katika malezi yao walipokuwa watoto. Malezi kwa mtoto yanamchango mkubwa sana katika kujenga ama kuharibu afya ya akili ya mtoto.
  • Matukio ya kuhuzun

3. Kijamii

  • Matukio kama vile kukosa ajira, matatizo sehemu za kazi, kufukuzwa kazi/chuo, migogoro kazini au kustaafu kazi, kukosa mtoto, kuhamishwa mahali pa kazi, kuoa ama kuolewa.
  • Majanga kama vile kimbunga, mafuriko, tetemeko la ardhi, n.k.
  • Changamoto za kila siku za maisha kama vile talaka, mimba kuharibika, kutoa mimba, kutengana, kufungwa, kuuguza au kuugua muda mrefu, n.k.
  • Madeni, upweke, kukataliwa, kujuta vinaweza kusababisha ugonjwa wa sonona.

Matibabu ya Ugonjwa wa Sonona

Sonona ni ugonjwa unaotibika. Ni muhimu sana kuwahi hospitali au kuonana na mtaalamu husika katika hatua za awali kabisa ili kuzuia kukithiri kwa tatizo. Matibabu ya ugonjwa wa sonona yanagawanyika katika sehemu kuu mbili; ambazo ni:

1. Tiba ya Mazungumzo (Non-Pharmacological)

Mazungumzo na mtaalamu wa afya ya akili ni mojawapo ya tiba madhubuti kwa wagonjwa wa sonona. Njia hii haihusishi dawa ikiwa na maana ya vidonge wala sindano. Hii ni tiba ya kisaikolojia ikiwa na lengo la kubadilisha mtazamo wa muathirika.

2. Tiba ya Kutumia Dawa (Pharmacological)

Hii ni njia inayohusisha utumiaji wa vidonge kama vile amitriptyline, fluoxetine, lorazepam, n.k. Dawa hizi zinafanya kazi katika ubongo kwenye sehemu inayohusika na kupandisha ama kushusha kemikali katika mwili ili kuleta mabadiliko ya kihisia na kitabia kwa mgonjwa husika. Njia hizi zinaweza kutumika zote kwa pamoja kwa mgonjwa mmoja pia.

Njia ya Kuzuia Ugonjwa wa Sonona

Sonona Kazini – Hiki ni kitabu kilichoandikwa katika lugha ya Kiswahili nyepesi na yenye kueleweka na kinachoakisi uhalisia kwa lengo la kujifunza kwa undani zaidi juu ya ugonjwa huu wa sonona na namna gani unaweza kuepuka katika maisha yetu ya kila siku. Kitabu hiki ni kwa ajili ya kila mtu mwenye utashi wa kutambua changamoto anazopitia, aidha akiwa jinsia ya kike au ya kiume.

Credits: Dr. Grace Mapunda