Atolewa Uvimbe wenye Kilo Nne na Nusu,hali iliyomtesa kwa miaka 30
Madaktari Bingwa wa Rais Samia wamefanya upasuaji na kutoa uvimbe wenye uzito wa kilo 4 na nusu ambao uliomtesa mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa miaka 30.
Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Costantine Alloyce ambaye alikuwa akitoa huduma za kibingwa na madaktari wengine wa Rais Samia Halmashauri ya wilaya Morogoro kuanzia Juni 9-14, 2025 mkoani Morogoro.
“Juni 12, 2025 tulipata mgonjwa wa jinsia ya kiume mwenye umri wa miaka 61 mkazi wa kijiji cha mvuha halmashauli ya wilaya ya morogoro ambaye amekuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye korodani yake ya kushoto kwa takribani miaka 30,”amesema Dkt. Alloyce.
Amesema mgonjwa huyo amekuwa akihudhuria hospitali mbalimbali hasa vituo vya afya katika halmashauri hiyo na hospitali za wilaya takribani 3 bila kupata msaada na uvimbe huo ambao umepelekea kupungua ubora wa maisha yake ikiwa pamoja na kutofanikiwa kupata watoto.
Dkt. Aloyce amesema baada ya kumfanyia uchunguzi wa awali uvimbe ulionekana kuwa mgumu, wenye umbo la tufe na urefu wa kipenyo chake kilikuwa sentimita 20 na ulikuwa unampa maumivu lakini haukuwa na maji ndani yake na korodani ya kushoto ilikuwa imemezwa na uvimbe huo.
Ameongeza kuwa Korodani ya kulia ilikuwepo lakini ilikuwa imezungukwa na maji, hivyo baada vipimo walimfanyia upasuaji.
Huduma hizo kwa mkoa wa Morogoro zilianza kutolewa Juni 9, 2025 mpaka Juni 14, 2025 zikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakipata changamoto za kupata huduma za kibingwa kutokana na umbali wa mahali zinapopatikana hudumu za kibingwa na bingwa bobezi au kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu.
REPLY HAPA
image quote pre code