Mamlaka nchini Israel zimethibitisha watu zaidi ya 20 wamejeruhiwa

Mamlaka nchini Israel zimethibitisha watu zaidi ya 20 wamejeruhiwa

#1

Hii ni kufuatia mashambulizi na Iran,Kisha kutangaza kusitisha kwa muda safari za anga nchini humo hadi pale itakapotangazwa vinginevyo.



Tehran. Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limethibitisha kutekeleza mashambulizi ya anga maeneo mbalimbali nchini Israel ikiwemo shambulizi lililolenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion, vituo vya utafiti na kambi za msaada wa kijeshi nchini humo.

Shirika la Habari la Tasnim nchini Iran limeripoti kuwa mashambulizi hayo ya IRGC nchini Israel yametekelezwa asubuhi ya leo Jumapili Juni 22, 2025.

Mashambulizi hayo yametekelezwa zikiwa zimepita saa chache tangu Marekani ishambulie vinu vya nyuklia vya Iran vilivyoko maeneo ya Fordow, Natanz na Isfahan.

Mamlaka nchini Israel zimethibitisha watu zaidi ya 20 wameshajeruhiwa kufuatia  mashambulizi hayo na kutangaza kusitisha kwa muda safari za anga nchini humo hadi pale itakapotangazwa vinginevyo.

Kutokana na mashambulizi hayo ya Iran yamewalazimisha watu zaidi ya 10,000 kuhama makazi yao hususan walikuwa kwenye jijini Tel viv, huku takriban watu 32,000 wakiwasilisha maombi kwa Serikali wakitaka fidia kwa uharibifu wa nyumba au mali zao.

Taarifa hiyo imesema mashambulizi hayo yalijumuisha matumizi ya makombora ya masafa marefu yenye vimiminika maarufu kama ‘solid-fuel’.

Pia Jeshi la Israel (IDF) limedai kuwa Iran katika mashambulizi ya leo asubuhi imetumia kombora jipya la hali ya juu la ‘Kheybar-Shekan’. 
IDF imesema Iran ilirusha makombora kwa awamu mbili ambayo ni jumla ya makombora 27 ambapo katika awamu ya kwanza yamerushwa makombora 22 na matano katika awamu ya pili.



Maeneo yaliyolengwa yalikuwa makubwa, kuanzia ukingo wa Golan unaokaliwa kwa nguvu, Galilaya hadi maeneo ya pwani ya kaskazini na kati. 

IDF imesema maeneo 10 tofauti yameathirika, ama moja kwa moja kutokana na makombora hayo hasa maeneo ya Jiji la Tel Aviv na Haifa. 

IDF pia imetangaza kuwa baada ya mashambulizi hayo ya Iran, nayo imejibu kwa kushambulia magharibi mwa nchi hiyo huku ikilenga maeneo ya kijeshi.

‘Hakuna tishio la uranium’

Iran yatuliza tena wananchi kuhusu hofu ya mionzi ya nyuklia.
Mohammad Reza Kardan, Naibu Mkurugenzi wa  Mamlaka ya Udhibiti wa Nyuklia nchini Iran amesema kuwa “hakuna mionzi au uchafuzi wa mionzi ya nyuklia ulioonekana nje ya maeneo au vituo vilivyoshambuliwa na mashambulizi ya anga ya Marekani.”

“Mipango ya awali ilikuwepo na hatua zilichukuliwa ili kulinda usalama na afya ya wananchi wapendwa wa nchi, na licha ya mashambulizi ya kikatili ya asubuhi ya leo katika vituo vya nyuklia, kutokana na maandalizi yaliyokuwepo awali na hatua zilizochukuliwa, hakuna mionzi ya nyuklia iliyoonekana nje ya maeneo haya,” alisema Kardan, kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA.

“Wananchi wanaweza kuendelea na maisha yao ya kawaida katika maeneo ya karibu na vituo hivyo bila hofu yoyote,” aliongeza.

Iran yamuua jasusi wa Mossad

Wakati mataifa hayo yakiendelea kushambuliana kwa makombora, Iran imetangaza kumnyonga Ofisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) Majid Mosayebi.

Mosayebi alishtakiwa na kukutwa na hatia kwa makosa ya kufanya ujasusi nchini Iran ambapo mahakama nchini humo ilimuhukumu kifo kwa kunyongwa. Chombo cha Habari nchini Iran cha Mizan Online kimethibitisha adhabu hiyo kutekelezwa.

“Majid Mosayebi … alinyongwa asubuhi ya leo baada ya kupitia mchakato mzima wa kesi ya jinai na baada ya hukumu yake kuthibitishwa na Mahakama Kuu,” Mizan iimeripoti.
Ilidaiwa kuwa Mosayebi alitaka kutoa taarifa nyeti kwenda Shirika la ujasusi la Mossad la Israel.

Iran italipaje kisasi kwa Marekani?

Katika mahojiano ya Al Jazeera na Mkurugenzi wa masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha San Francisco, Stephen Zunes kuhusiana na jinsi anavyotarajia Iran kujibu mashambulizi ya Marekani alisema, 

 “wana chaguzi kadhaa. Wanaweza kushambulia vikosi vya Marekani moja kwa moja. Kuna hadi Wamarekani 40,000 walioko ndani ya maeneo yanayoweza kufikiwa kirahisi mashariki ya kati, si tu ya makombora ya Iran bali pia ndege zisizo na rubani na silaha nyingine.

“Kuna meli za kijeshi katika Ghuba ya Uajemi, karibu na pwani ya Iran. Nazo pia zinaweza kuwa hatarini ikiwa zitashambuliwa… jambo hili linaweza kuathiri usafirishaji wa kimataifa, bei ya mafuta na kwa kweli uchumi mzima wa dunia.

“Kuna pia wanamgambo wa kujihami (proxy militias) nchini Iraq ambao wanaweza kulenga kambi za Marekani huko.

Zunes ameongeza: “Hivyo kuna njia nyingi ambazo vikosi vya Marekani vinaweza kuwa hatarini, na nitashangaa kama Iran haitalenga baadhi ya hivi.” 

Oman, Qatar na Iraq zajitosa

Taifa la Oman ambalo limekuwa likisaidia kusuluhisha mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu nyuklia kati ya Marekani na Iran, limelaani mashambulizi ya Marekani nchini Iran huku likiita kitendo hicho ni haramu cha uchokozi.

Shirika rasmi la Habari la Oman lilimnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje akisema kuwa Sultani wa Oman, Haitham bin Tariq ana wasiwasi na kitendo hicho huku akisema kitachochea zaidi mzozo huo jambo ambalo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Qatar nayo haijakaa kimya, imesema mvutano huo ni hatari kufuatia mashambulizi ya Marekani huku ikisema utasababisha madhara makubwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa. 

Wakati huo, Iraq, imeeleza wasiwasi wake na kulaani kulengwa kwa vituo vya nyuklia vya Iran, na kusema kuwa kuongezeka kwa hali ya kijeshi ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kanda.

REPLY HAPA


image quote pre code