TAHADHARI; Nchi 5 kati ya nchi 13 zenye njaa kali duniani

TAHADHARI; Nchi 5 kati ya nchi 13 zenye njaa kali duniani

#1

TAHADHARI; Nchi 5 kati ya nchi 13 zenye njaa kali duniani 



Ripoti mpya ya pamoja ya Umoja wa Mataifa inaonya kuwa watu katika nchi 5 kati ya nchi 13 zenye njaa kali duniani wako kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na njaa kali, vifo na maafa ikiwa msaada wa kibinadamu hautatolewa haraka na juhudi za kimataifa hazitaelekezwa kukomesha migogoro, kupunguza uhamishaji wa kulazimishwa na kuongeza msaada wa haraka kwa kiwango kikubwa.

Ripoti hiyo mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO na la Mpango wa chakula duniani, WFP, inaonesha kuwa Sudan, Palestina, Sudan Kusini, Haiti na Mali ni maeneo yenye wasiwasi mkubwa zaidi, ambapo jamii tayari zinakabiliwa na baa la njaa au viwango vya juu sana vya uhaba wa chakula kutokana na migogoro inayoendelea au kuongezeka, mishtuko ya kiuchumi na majanga ya asili. Hali hizi zimekuwa mbaya zaidi kutokana na vikwazo vya upatikanaji wa misaada na upungufu mkubwa wa ufadhili.

Taarifa iliyotolewa leo Roma, Italia hutolewa mara mbili kwa mwaka na hutumika kama tahadhari ya mapema na uchambuzi wa utabiri wa mwelekeo wa hali ya chakula kwa miezi mitano ijayo. Toleo hili, lililoandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka Muungano wa Ulaya kupitia Mtandao wa Kimataifa Dhidi ya Majanga ya Chakula (GNAFC), linatabiri hali kuwa mbaya zaidi ya uhaba mkubwa wa chakula katika nchi na maeneo 13.

Maeneo ya wasiwasi mkubwa zaidi

Sudan: Njaa ilithibitishwa mwaka jana 2024 na hali inaendelea kuwa mbaya kutokana na vita na ufurushaji unaoendelea, hasa katika maeneo ya Kordofan na Darfur. Takriban watu milioni 24.6 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula (IPC Hatua ya 3 au zaidi), wakiwemo watu 637,000 katika hali ya maafa (IPC Hatua ya 5).

Palestina (Ukanda wa Gaza): Uwezekano wa baa la njaa unaongezeka kutokana na operesheni kubwa za kijeshi zinazozuia utoaji wa msaada muhimu. Watu wote 2.1 milioni wanakadiriwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, wakiwemo 470,000 walio katika hatari ya njaa kali (IPC Hatua ya 5) hadi Septemba 2025.

Sudan Kusini: Inakumbwa na changamoto mseto za kisiasa, hatari ya mafuriko, na hali ngumu ya kiuchumi. Watu takriban milioni 7.7 (asilimia 57 ya idadi ya watu) wanakabiliwa na njaa kali, huku 63,000 wakiwa kwenye hatari ya njaa ya maafa.

Haiti: Ukatili wa magenge umeongezeka na kuzuia misaada. Takriban watu 8,400 waliopo katika mji Mkuu, Port-au-Prince tayari wanakabiliwa na njaa ya maafa (IPC Hatua ya 5) kufikia Juni 2025.

Mali: Bei za juu za nafaka na mapigano yanaathiri uwezo wa familia kujimudu. Watu 2,600 wanakabiliwa na hatari ya njaa kali (CH Hatua ya 5) kati ya Juni hadi Agosti 2025 iwapo msaada hautatolewa kwa wakati.

Maeneo mengine ya wasiwasi

Yemen, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Myanmar, na Nigeria: Zina hitaji la haraka la msaada ili kuokoa maisha.

Burkina Faso, Chad, Somalia, Syria: Zinaendelea kuwa maeneo ya hatari.

REPLY HAPA


image quote pre code