Mohamed Shaib Saleh, mkazi wa Pemba, ameokolewa salama baada ya kujirusha baharini kutoka kwenye boti ya Zanzibar 3 iliyokuwa safarini kutoka Pemba kuelekea Unguja.
Tukio hilo limetokea leo Juni 17, 2025 saa 2:15 asubuhi, baada ya boti kuvuka eneo maarufu la mkondo wa Nungwi.
Baada ya kujirusha, boti iligeuka kurudi eneo alilojirusha. Mohamed akarushiwa vifaa maalumu vya uokozi, kisha baharia mmoja alijirusha kumfuata na kumwokoa kwa mafanikio.
Chausiku Shija ni mmoja wa mashuhuda waliokuwa wamekaa na kijana huyo wakati anajirusha majini. “Yule kijana alikuja kwanza pale akasimama wakawa wanapiga stori na babu mmoja, kisha akavua viatu na soksi akaenda msalani kutia udhu kisha akaenda humo msikitini kuswali.
“Alipomaliza akaja palepale, akamuuliza babu, hivi kwenye mkondo wa Nungwi tushafika? Yule babu akamweleza, Zamani tumeshapita, ndio hapo akaruka mara moja. Aliporuka tukapiga kelele kuna mtu karukia majini.
Tatu Khamis Ali mkazi wa Mwera amesema: “Mimi nilikuwa nimelala, lakini nikasikia watu wanaongea na kuulizana, baada ya hapo nikasikia kelele nyingi kwamba kachupa, nami niliona tu mkono,"
Shuhuda mwingine Rashid Sultan Rashid amesema, “yule bwana alikuja kwa nguvu kama anataka kuanguka huko nikamwambia angalia usije kuanguka, kasema sianguki nipo fiti, baadaye tukakaa akaniuliza kama tumeshavuka Nungwi, nikamwambia tayari:
Amesema alipomwambia wameshavuka Nungwi akawa anabisha kwamba yeye Nungwi anayoitaka bado hajafika, kwa hiyo baadaye tukaenda kusali ila alinitangulia kutoka na ndio hapo nikasikia kelele amejirusha kwenye maji.
Kapteni wa boti hiyo Mohamed Ali Khamis amesema alipokea taarifa ya mtu kujitosa baharini na alichofanya ni kusimamisha injini na aliwaamuru mabaharia warushe jaketi la kujiokoa.
"Nashukuru Mungu yule mtu tumemuokoa ndani ya dakika 15 na yupo salama," amesema.
Amesema wamefanikiwa kwa haraka kwa sababu ya umakini na vifaa walivyonavyo.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, Mtumwa Said amethibitisha kutokea tukio hilo ikiwamo kufanyika jitihada za haraka kumuokoa kijana huyo.
REPLY HAPA
image quote pre code