Shirika la Afya Duniani (WHO) leo limetoa mwongozo wake wa kwanza kabisa wa kimataifa kuhusu usimamizi wa ugonjwa wa seli mundu (SCD) wakati wa ujauzito, likishughulikia changamoto kubwa na inayoongezeka ya kiafya inayoweza kuwa hatari kwa maisha ya wanawake na watoto wao.
SCD ni kundi la magonjwa ya kurithi ya damu yanayotokana na seli nyekundu za damu zilizo na umbo lisilo la kawaida linalofanana na nusu mwezi au mundu. Seli hizi zinaweza kuziba mzunguko wa damu, na kusababisha upungufu mkali wa damu, maumivu makali ya mara kwa mara, maambukizi ya kurudia, pamoja na hali za dharura za kiafya kama vile kiharusi, sepsis (kinga za mwili zinapopambana na mwili) au kushindwa kwa viungo.
Hatari za kiafya zinazohusiana na SCD huongezeka wakati wa ujauzito, kutokana na mahitaji makubwa ya oksijeni na virutubisho mwilini. Wanawake wenye SCD wako katika hatari kubwa kwa kati ya mara 4 hadi 11 zaidi ya kufariki dunia wakati wa ujauzito ikilinganishwa na wanawake wasio na hali hiyo. Pia wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya uzazi kama vile shinikizo la damu la ujauzito (pre-eclampsia), na watoto wao wako katika hatari ya kufa tumboni, kuzaliwa kabla ya muda au kuwa na uzito mdogo.
“Kwa huduma bora za afya, wanawake wenye magonjwa ya kurithi ya damu kama seli mundu wanaweza kuwa na ujauzito na kujifungua salama,” amesema Dkt Pascale Allotey, Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi na Utafiti katika WHO na Mpango Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Uzalianaji wa Binadamu (HRP). “Mwongozo huu mpya unalenga kuboresha matokeo ya ujauzito kwa wale walioathiriwa. Kwa kuongezeka kwa visa vya seli mundu, uwekezaji zaidi unahitajika haraka ili kupanua upatikanaji wa matibabu ya kisayansi wakati wa ujauzito pamoja na uchunguzi na taarifa kuhusu ugonjwa huu uliopuuzwa kwa muda mrefu.”
Kuna takriban watu milioni 7.7 wanaoishi na SCD duniani kote, idadi ambayo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 tangu mwaka 2000. Inakadiriwa kuwa SCD husababisha vifo zaidi ya 375,000 kila mwaka. Ugonjwa huu umeenea zaidi katika maeneo yenye malaria, hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo kuna takribani visa 8 kati ya 10 pamoja na sehemu za Mashariki ya Kati, Karibea, na Asia Kusini. Kutokana na uhamaji wa watu na kuongezeka kwa umri wa kuishi, jeni ya seli mundu sasa inasambaa zaidi duniani, na hivyo kuhitaji wahudumu wa afya ya uzazi kufahamu namna ya kusimamia ugonjwa huu.
Hadi sasa, mwongozo wa kimatibabu kuhusu usimamizi wa SCD wakati wa ujauzito umeegemea zaidi kwenye taratibu za nchi tajiri. Mwongozo huu mpya wa WHO unalenga kutoa mapendekezo ya kisayansi yanayofaa pia kwa mazingira ya kipato cha chini na cha kati, ambapo visa na vifo vingi hutokea. Kwa hivyo, mwongozo unajumuisha mapendekezo zaidi ya 20 yanayohusisha:
matumizi ya foliki asidi na virutubisho vya madini ya chuma, ikiwa ni pamoja na marekebisho kwa maeneo yenye malaria;
usimamizi wa hali ya dharura za seli mundu na kupunguza maumivu;
kuzuia maambukizi na kuganda kwa damu;
matumizi ya mfululizo ya kuongezewa damu kwa tahadhari; na
ufuatiliaji wa ziada wa afya ya mama na mtoto wakati wote wa ujauzito.
Mwongozo huu pia unasisitiza hitaji la huduma ya heshima, ya mtu binafsi, inayozingatia mahitaji maalum, historia ya matibabu na mapendeleo ya wanawake. Pia unagusia umuhimu wa kupambana na unyanyapaa na ubaguzi katika mazingira ya huduma ya afya, changamoto kubwa kwa watu wenye SCD katika nchi nyingi duniani.
“Ni muhimu sana wanawake wenye seli mundu waweze kujadili mapema chaguo la huduma zao za afya wakati wa ujauzito au hata kabla ya hapo na watoa huduma wenye uelewa wa hali yao,” amesema Dkt Doris Chou, Afisa wa Matibabu na mwandishi mkuu wa mwongozo huo. “Hii inawawezesha kufanya maamuzi yenye taarifa kuhusu chaguzi za matibabu, na pia kukubaliana jinsi ya kushughulikia matatizo yanayoweza kujitokeza, ili kuboresha matokeo kwa mama, ujauzito na mtoto wake.”
Kwa kuzingatia ugumu wa hali hizi, iwapo mwanamke mjamzito ana SCD, mwongozo unaeleza umuhimu wa kuwa na timu ya wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika huduma yake. Hii inaweza kujumuisha wataalamu wa damu (haematologists), wakunga, madaktari wa watoto na magonjwa ya wanawake na uzazi.
Seli mundu ni hali ya kiafya iliyopuuzwa ambayo bado haijapewa fedha na utafiti wa kutosha licha ya kuongezeka kwake duniani kote. Ingawa chaguzi za matibabu zinaimarika kwa jamii kwa ujumla, mwongozo unasisitiza haja ya haraka ya kufanya utafiti zaidi kuhusu usalama na ufanisi wa matibabu ya SCD kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha—makundi ambayo kihistoria yamekuwa yakitengwa kwenye majaribio ya kimatibabu.
Chapisho hili ni la kwanza katika mfululizo mpya wa WHO kuhusu usimamizi wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza wakati wa ujauzito. Miongozo ijayo itashughulikia hali za moyo na mishipa, kisukari, magonjwa ya kupumua, matatizo ya afya ya akili na matumizi ya vilevi. Magonjwa sugu yanatambuliwa kwa kiwango kikubwa kama wachangiaji wa vifo na magonjwa kwa mama na watoto wachanga.
REPLY HAPA
image quote pre code