Dkt. Mwigulu Nchemba Awakilisha Tanzania Mkutano wa AfDB Congo

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amewasili mjini Brazzaville, nchini Jamhuri ya Kongo kushiriki Mkutano wa 61 wa Mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), unaowakutanisha viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka barani Afrika na duniani.

Dkt. Mwigulu anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo mkubwa unaofanyika Mei 26 hadi 27, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kintele, jijini Brazzaville.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maya Maya, Waziri Mkuu huyo alipokelewa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Anatole Collinet Makosso, ikiwa ni ishara ya umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo wa kimataifa.

Mkutano wa AfDB mwaka huu unajadili masuala muhimu ya maendeleo ya Afrika, hususan namna ya kuimarisha uchumi wa bara hilo, kuongeza uwekezaji, pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto za kifedha zinazozikabili nchi mbalimbali za Afrika.

Aidha, viongozi na wajumbe wanaoshiriki wanatarajiwa kujadili mikakati ya kuongeza upatikanaji wa rasilimali za fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, miundombinu, biashara na uwekezaji ili kukuza uchumi endelevu wa bara la Afrika.

Zaidi ya wajumbe 3,000 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo, wakiwemo Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za Afrika, watunga sera, taasisi za kifedha, wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na washirika wa maendeleo kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unaonyesha nafasi yake katika majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo ya uchumi wa Afrika na ushirikiano wa kifedha kati ya nchi wanachama wa AfDB.

...See more

WEKA COMMENT YAKO HAPA(MAONI)KUHUSU MADA HII

Related Discussions...