Kampuni kubwa ya teknolojia ya imetangaza rasmi kuzindua huduma mpya za usajili wa kulipia kwa majukwaa yake maarufu ya Facebook, Instagram pamoja na Whatsapp , hatua inayotajwa kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wa mapato wa kampuni hiyo ambao kwa muda mrefu ulitegemea matangazo ya biashara.

Huduma hizo mpya zitafahamika kwa jina la “Plus” na zinatarajiwa kuwapa watumiaji uwezo wa kufurahia vipengele vya ziada vya ubinafsishaji wa akaunti, kuongeza uonekano wa machapisho pamoja na zana maalumu za kuongeza ushirikishwaji wa hadhira kwenye majukwaa hayo.

Kwa mujibu wa Meta, huduma ya Instagram Plus na Facebook Plus zitagharimu dola 3.99 kwa mwezi kila moja, huku WhatsApp Plus ikigharimu dola 2.99 kwa mwezi. Kampuni hiyo inaamini huduma hizo zitawavutia zaidi watumiaji wanaotaka uzoefu wa kipekee na wa kisasa zaidi kwenye mitandao ya kijamii.

Instagram Plus itakuja na maboresho kadhaa mapya yakiwemo uwezo wa kuongeza muda wa kuonekana kwa Instagram Stories zaidi ya saa 24, kuona mara ambazo Story imetazamwa tena pamoja na uwezo wa kuangalia Stories kwa siri bila kuonekana kwenye orodha ya waliotazama. Watumiaji pia wataweza kuangaziwa Stories zao kila wiki ili kuongeza uonekano kwa wafuasi wao.

Mbali na hayo, huduma hiyo italeta zana mpya za ubinafsishaji wa akaunti kama fonti maalumu, ikoni tofauti za programu, pini za ziada kwenye wasifu pamoja na miitikio mipya ya “Super Heart” ambayo itawaruhusu watumiaji kuonyesha hisia zao kwa namna ya kipekee zaidi.

Kwa upande wa Facebook Plus, huduma hiyo inalenga kuongeza ushirikishwaji wa watumiaji kwa kuwapa uwezo wa kuboresha muonekano wa wasifu wao, kuongeza ufikaji wa machapisho pamoja na kutumia vipengele vya kipekee visivyopatikana kwa watumiaji wa kawaida.

Huduma ya WhatsApp Plus nayo italeta maboresho makubwa kwenye mfumo wa ujumbe na muonekano wa programu. Watumiaji wataweza kutumia sauti maalumu za arifa, mandhari tofauti za WhatsApp, stika za kipekee pamoja na uwezo wa kubandika mazungumzo mengi zaidi kwa wakati mmoja. Pia kutakuwa na zana mpya za kupanga mawasiliano kwa urahisi zaidi.

Meta imesisitiza kuwa huduma hizi mpya hazitachukua nafasi ya huduma yake ya sasa ya Meta Verified ambayo inalenga uthibitisho wa akaunti, ulinzi dhidi ya watu wanaojifanya wengine pamoja na huduma za msaada kwa wateja.

Hatua hiyo inakuja wakati kampuni hiyo ikiendelea kuongeza uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya akili unde (AI). Ripoti zinaonyesha kuwa Meta inatarajiwa kutumia hadi dola bilioni 145 mwaka huu kwa ajili ya vituo vya data na miundombinu ya AI ili kuimarisha ushindani wake kwenye sekta ya teknolojia duniani.

Wakati huohuo, Meta inaendelea kufanya majaribio ya huduma nyingine mpya ya usajili inayojulikana kama “Meta One”, ambayo inalenga watengenezaji wa maudhui, biashara pamoja na watumiaji wa Meta AI.

Kwa kufanya hivyo, Meta sasa inaungana na kampuni nyingine za mitandao ya kijamii kama kupitia pamoja na kupitia ambazo tayari zina huduma za usajili wa kulipia kwa watumiaji wao.

Wachambuzi wa teknolojia wanaamini kuwa mabadiliko haya yanaweza kuwa mwanzo wa zama mpya ambapo kampuni nyingi za mitandao ya kijamii zitategemea zaidi huduma za usajili badala ya matangazo pekee ili kuongeza mapato yao.

...See more

1 Comments

  1. Dunia inaenda kwa Kasi sana,Teknolojia zinapanuka kwa kiwango kikubwa sana,Mfumo wa AI ni kitu kingine kimekuja kwa Kasi kubwa sana, Sio Mchezo kwa kweli!!!

    ReplyDelete

Post a Comment

Mijadala Inayoendelea