Nicki Minaj Afunguka Kumkubali Trump, Asema Mastaa Wengi Wanaogopa Kusema Ukweli
Msanii maarufu wa Hip Hop Nicki Minaj amezua mjadala mkubwa duniani baada ya kuweka wazi msimamo wake wa kumuunga mkono Donald Trump huku akidai kuwa mastaa wengi wa burudani wana mawazo kama yake lakini wanaogopa kuyasema hadharani.
Katika mahojiano yaliyofanywa na jarida la Time na kuchapishwa Mei 13, 2026, Nicki Minaj alisema kuwa kwa muda mrefu alikuwa akimuunga mkono Trump kimya kimya kutokana na hofu ya kushambuliwa na kukosolewa ndani ya tasnia ya muziki na burudani.
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema mazingira ya tasnia ya burudani nchini Marekani yamejengwa zaidi kuunga mkono chama cha Democrats jambo ambalo huwafanya wasanii wengi kushindwa kueleza hisia zao za kisiasa kwa uhuru.
Kwa mujibu wa Minaj, kuna wasanii wengi maarufu wanaokubaliana na mawazo yake kuhusu siasa lakini hawapo tayari kuzungumza wazi kwa kuhofia kupoteza mashabiki, mikataba ya kazi au kuonekana tofauti na wenzao katika tasnia hiyo.
“Nahitaji kuwa mmoja wa watu watakaobeba lawama ili wengine wapate ujasiri wa kusema wanachokiamini,” alisema Minaj katika mahojiano hayo yaliyoibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mbali na kumuunga mkono Trump, Minaj pia alimpongeza rais huyo wa zamani kwa kile alichokiita mvuto wa kipekee wa kisiasa na kijamii. Alisema Trump ana “vibe yake mwenyewe” na akamlinganisha na muigizaji maarufu wa zamani Marilyn Monroe kutokana na uwezo wake wa kuvutia watu na kubaki gumzo kila wakati.
Katika mazungumzo hayo, Nicki Minaj hakusita kuwataja baadhi ya watu wakubwa katika siasa na muziki. Alimkosoa aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama pamoja na rapper maarufu Jay-Z akidai kuwa baadhi ya rappers hawampendi Jay-Z lakini hawawezi kusema ukweli huo hadharani kwa sababu ya ushawishi wake mkubwa kwenye tasnia ya muziki.
Minaj pia alifunguka kuhusu matukio ya “swatting” yaliyowahi kutokea nyumbani kwake mjini Los Angeles ambapo watu walitoa taarifa za uongo kwa polisi na kusababisha vikosi vya usalama kuvamia nyumba yake. Msanii huyo alisema msaada alioupata kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama cha Republican ulimfanya abadili mtazamo wake kuhusu siasa na kuamua kuzungumza kwa uwazi zaidi.
Kauli za Nicki Minaj zimeendelea kugawa maoni ya mashabiki duniani, huku baadhi wakimsifu kwa ujasiri wake wa kueleza anachoamini na wengine wakimkosoa kwa kuingiza siasa katika tasnia ya burudani. Hata hivyo, hatua yake ya kuzungumza wazi imeongeza mjadala mpana kuhusu uhuru wa maoni miongoni mwa wasanii wa Marekani na namna siasa zinavyoathiri maisha ya watu maarufu.

.jpeg)



Post a Comment
Related Discussions...