Trump Aionya Iran: “Muda Unakwisha” Wakati Mazungumzo ya Amani Yakikwama
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo jipya kali kwa Iran akisema kuwa “muda unakwisha” huku mazungumzo ya amani kati ya pande hizo yakiripotiwa kukwama.
Trump aliandika ujumbe huo kupitia mtandao wake wa Truth Social siku ya Jumapili, akisisitiza kuwa Iran inapaswa kuchukua hatua haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi.
“Nchini Iran, saa inaendelea kuhesabu muda, na ni bora wakachukua hatua haraka, vinginevyo hakutakuwa na chochote kitakachosalia,” aliandika Trump. “Muda ni muhimu!”
Kauli hiyo imekuja wakati Trump akitarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kujadili hali ya usalama na maendeleo ya hivi karibuni katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Axios, viongozi hao walijadili suala la Iran huku timu ya usalama wa taifa ya Trump ikitarajiwa kukutana siku ya Jumanne kujadili hatua zinazofuata.
Vyombo vya habari vya Iran vilidai kuwa serikali ya Trump haijatoa mapendekezo yenye masharti nafuu wala maridhiano ya maana kufuatia mapendekezo ya karibuni yaliyotolewa na Tehran, jambo lililoongeza hofu kuwa mazungumzo hayo yanaweza kuvunjika kabisa.
Onyo hilo pia limekuja baada ya Trump kueleza kuwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano yako katika hali mbaya sana, huku akiitaja pendekezo la Iran kama “halikubaliki kabisa.”
Wakati huo huo, serikali ya Marekani inaendelea kupata presha ya kumaliza mzozo huo kutokana na athari za kiuchumi zinazozidi kuonekana nchini humo, hasa kupanda kwa bei ya mafuta. Ripoti zinaonyesha bei ya mafuta imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 hadi kufikia wastani wa dola 4.51 kwa galoni moja nchini Marekani.
Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth naye alikwepa kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu gharama halisi ya mzozo huo alipokuwa akizungumza mbele ya wabunge mjini Capitol Hill.
Katika kikao hicho cha bajeti ya Pentagon, Pete Aguilar kutoka California alihoji kuhusu matumizi yanayoongezeka ya vita hivyo, huku afisa wa Pentagon Jay Hurst akieleza kuwa gharama zimeongezeka kutoka dola bilioni 25 hadi dola bilioni 29.
Hurst alisema ongezeko hilo limetokana na gharama za ukarabati na uingizwaji wa vifaa vya kijeshi pamoja na matumizi ya kawaida ya operesheni za kijeshi zinazoendelea katika eneo la mapigano.
Mvutano huo unaendelea kuzua wasiwasi duniani kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa machafuko makubwa katika Mashariki ya Kati ikiwa juhudi za kidiplomasia zitashindwa kufikia makubaliano.






Post a Comment
Related Discussions...