Watumiaji wa WhatsApp Wazua Hofu Kuhusu Faragha ya Status Baada ya Kuonekana kwa Namba Zisizohifadhiwa(Unsaved number)


Watumiaji wa WhatsApp wameendelea kueleza wasiwasi wao kwenye mitandao ya kijamii baada ya kugundua kuwa baadhi ya watu ambao hawajahifadhiwa kwenye simu zao(Unsaved numbers) wanaonekana kuweza kuona “Status” zao.

Malalamiko hayo yamezua mjadala mkubwa kuhusu faragha na usalama wa taarifa binafsi ndani ya programu hiyo maarufu ya mawasiliano inayomilikiwa na Meta Platforms.

Watumiaji kadhaa kwenye mtandao wa X walieleza hali hiyo kuwa ya “kukera” na “kutia wasiwasi”, huku wengine wakijiuliza kama ni mabadiliko mapya ya mfumo au hitilafu ya kiufundi.

Mtumiaji mmoja alisema “Maboresho haya ya WhatsApp yanayoruhusu watu ambao sijawahifadhi kuona status zangu hayapendezi kabisa. Kama sina namba yako kwenye contacts zangu, hupaswi kuona status yangu.”

Naye mtumiaji mwingine, alisema hali hiyo imemfanya ajisikie kutokuwa salama mtandaoni.

“Update hii mpya ya WhatsApp siyo muhimu na inanifanya nijisikie vibaya. Kwa nini nione status za watu ambao sijawahifadhi? Je, nao wanaweza kuona zangu?” alihoji.

Wengine waliendelea kueleza hofu kuhusu namna taarifa zao zinavyoweza kuonekana kwa watu wasiowafahamu moja kwa moja.

Wakati huo huo, baadhi ya watumiaji walidai hata watu waliowazuia au kuwawekea vizuizi bado wanaweza kuona status zao, jambo lililoongeza taharuki zaidi.

Hata hivyo, WhatsApp imejitokeza kutuliza hofu hizo na kusisitiza kuwa hakuna mabadiliko yaliyofanyika kwenye mfumo wake wa msingi wa faragha.

Kupitia ukurasa wake rasmi kwenye X, kampuni hiyo ilisema kuwa ujumbe binafsi, simu pamoja na Status bado zinalindwa kwa teknolojia ya “end-to-end encryption”.

“Ujumbe wako binafsi, simu na Status zako zinalindwa kwa mfumo wa end-to-end encryption na hilo halijabadilika,” WhatsApp ilieleza.

Licha ya maelezo hayo, mjadala kuhusu faragha ya watumiaji umeendelea kushika kasi huku wengi wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu namna mfumo wa Status unavyofanya kazi, hasa kwa watu ambao hawajahifadhiwa kwenye orodha za mawasiliano.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...