Mchakato waanza ili kuwarudisha Watanzania waliopo Israel na Iran

Mchakato waanza ili kuwarudisha Watanzania waliopo Israel na Iran

#1

Serikali imeanza kuchukua hatua za haraka na za kiutendaji ili kuhakikisha Watanzania waliopo nchini Iran na Israel wanarejeshwa salama nchini.

Uamuzi huo umetokana na mgogoro unaoendelea kushamiri kati ya mataifa hayo mawili, hali ambayo imesababisha baadhi ya nchi kuanza kuchukua hatua za dharura za kuwarejesha raia wao waliopo katika maeneo hayo.

Mashambulizi yanayoendelea kati ya Taifa la Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalianza Juni 13, 2025 hali iliyochangia kuendelea kuzorota kwa usalama katika mataifa hayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo, Juni 19, 2025, Watanzania waliopo katika nchi hizo wamethibitishwa kuwa salama.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuwaorodhesha Watanzania waliopo katika nchi hizo kupitia balozi zake zilizoko Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (ambao unaiwakilisha Tanzania nchini Iran), Kuwait na Israel.

 “Taarifa zilizopo hadi sasa zinaonesha kuwa kuna Watanzania 168 waliopo nchini Iran, wakiwemo wanafunzi 134 katika mji wa Qom na wengine 34 jijini Tehran,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa upande wa Israel, inakadiriwa kuwa kuna zaidi ya Watanzania 200, wakiwemo watumishi wa Ubalozi wa Tanzania, wanafunzi, na wafanyakazi katika taasisi mbalimbali. Kati yao, takriban Watanzania 50 tayari wamejiandikisha ili kupatiwa msaada wa kurejea nyumbani."

 “Pamoja na changamoto za kiusalama zilizopo, Serikali inathibitisha kuwa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Israel halijaathirika na mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati mashambulizi hayo yalipotokea, hapakuwa na mtu yeyote ndani ya jengo hilo, na maofisa wa ubalozi pamoja na familia zao wote wapo salama.

Pia, Balozi zetu nchini Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu(U.A.E) zimekuwa zikiwasiliana na Watanzania waliopo katika maeneo ya Iran na Israel, zikiwataka kuchukua tahadhari za kiusalama, wakati Serikali ikiendelea kushughulikia masuala yanayohusu usalama wao ikiwa ni pamoja na mustakabali wao wa kurudi nyumbani,” imeelezwa.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wake wa ndani na nje ya nchi, inaendelea na taratibu za kiutendaji ili kuhakikisha Watanzania waliopo katika maeneo hayo hatarishi wanarejeshwa nyumbani salama.

Taarifa hii ya Serikali inakuja wakati ambao kumekuwa na taarifa za mashambulizi yanayofanyika kati ya nchi hizo mbili hali inayozidisha hofu kwa wananchi.

Awali kombora lililorushwa kutoka Iran lililenga jengo la hospitali kuu iliyopo kusini mwa Israel na kusababisha majeruhi kadhaa, huku yenyewe ikijibu kwa kushambulia mtambo wa urutubishaji nyuklia.

Ofisa kutoka Idara ya Dharura ya Israel, Magen David Adom ameieleza Associated Press kuwa makombora mengine ya Iran yalipiga kwenye majengo mawili jijini Tel Aviv nchini humo na kujeruhi watu.

Kombora hilo lilitua Kituo cha Matibabu cha Soroka, ambacho huwadumia wagonjwa wengi Kusini mwa Israel.

Taarifa ya hospitali hiyo ilieleza kuwa sehemu kadhaa za jengo hilo ziliharibiwa na kuna majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.

Hospitali hiyo ilifungwa kwa muda ili kuzuia wagonjwa kuingia isipokuwa wale waliopo kwenye hali mbaya. Haikufahamika mara moja idadi ya watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amelaani shambulio hilo na kuahidi kulipiza kisasi, akisema: "Madikteta wa Iran wataadhibiwa kulingana na gharama za matendo yao.

Hospitali nyingi nchini Israel zimekuwa katika mipango ya dharura tangu wiki iliyopita, ikiwemo kubadili sehemu za maegesho ya magari kuwa wodi na kuwahamisha wagonjwa chini ya ardhi (under ground floor), hasa waliowekewa mashine za kusaidia kupumua.

Israel nayo ilifanya mashambulizi ikiulenga mtambo wa urutubishaji nyuklia wa Arak, tukio linalotajwa kuwa shambulio hatari zaidi nchini humo ikiwa ni siku ya saba tangu kuanza kwa mvutano baina ya mataifa hayo.

Via Mwananchi.

REPLY HAPA


image quote pre code