Mvutano mkubwa kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na bilionea, Elon Musk
Wawili hao ambao kwa muda mrefu walionekana kuwa marafiki wa karibu na washirika wa kimkakati, sasa wamejikuta wakiwa mahasimu wakubwa katika vita ya maneno inayoibua sintofahamu nchini Marekani na duniani kwa ujumla.
Chanzo cha mvutano huo ni muswada mpya wa bajeti uitwao ‘Big Beautiful Bill’ uliowasilishwa na Trump, ambao Musk ameuita hadharani kuwa ni ‘aibu kubwa kwa taifa.’
Kupitia jukwaa lake la X (zamani Twitter), Musk alitupa kombora la maneno akisema: “Huu ni muswada mbaya zaidi niliouona, unapandisha deni la taifa kwa kasi ya kutisha."
Trump naye hakukaa kimya. Akitumia jukwaa lake la Truth Social, alimshambulia Musk kwa maneno makali akidai, ‘Elon amekasirika kwa sababu tumekata ruzuku za magari ya umeme na anajua hii itaumiza kampuni yake ya Tesla.’
Alienda mbali zaidi na kutishia kuvunja mikataba ya serikali na kampuni za Musk akisema: “Njia rahisi ya kuokoa mabilioni ya dola ni kufuta ruzuku na kandarasi za Elon.’
Mgogoro huo umekuwa kama moto wa kifuu kwani hauzimiki kwa maji. Hisa za kampuni ya Tesla zimeshuka kwa asilimia 14 kwa siku moja, jambo lililosababisha kupotea kwa thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 150 bilioni katika soko la hisa.
Aidha, SpaceX – kampuni ya anga ya Musk – ipo katika hatari ya kupoteza kandarasi muhimu na taasisi kama Nasa, ambazo thamani yake inakadiriwa kufikia dola 15.2 bilioni kwa upande wa Nasa na dola 5.8 bilioni kutoka Idara ya Ulinzi.
Kwa upande wake, Trump Media & Technology Group, kampuni inayosimamia mtandao wa Truth Social, nayo imekumbwa na mtikisiko katika soko la hisa. Hali hiyo imesababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama cha Republican, ambapo baadhi ya maseneta kama Rand Paul na Mike Lee wameonyesha kuunga mkono msimamo wa Musk, huku wengine wakibakia upande wa Trump.
Musk alikaribia kutoa tamko la kufunga huduma za Dragon Spacecraft – chombo kinachotumiwa na Nasa kusafirisha wanaanga kwenda Kituo cha Anga cha Kimataifa, lakini baadaye alirudi nyuma, akisema: “Sawa, hatutafuta Dragon.”
Athari zinazoshika mizizi, mbali na mvutano huo kuwa wa maneno, athari zake zimeanza kushika mizizi ya kiuchumi na kisiasa.
Tesla sasa inakosa soko kutokana na kuondolewa kwa punguzo la kodi la dola 7,500 kwa wateja wa magari ya umeme. Hali hii imewaacha Wachina – hususan kampuni ya BYD – wakiwa washindi, baada ya kuipita Tesla kwa mauzo ya magari ya umeme barani Ulaya na Asia, mwaka 2024.
Kwa upande wa kisiasa, muswada wa bajeti wa Trump sasa uko shakani kupitishwa kwenye seneti kutokana na mpasuko uliosababishwa na mzozo huu. Mpatanishi bilionea Bill Ackman amejaribu kuwapatanisha wawili hawa, lakini hadi sasa juhudi hizo zimeonekana kugonga mwamba.
Wengi wanasubiri kuona ni nani atashinda vita hii ya maneno na jeuri. Ikiwa maridhiano hayatafikiwa, Marekani inaweza kushuhudia mgawanyiko mkubwa wa kiuchumi na kisiasa unaoweza kuvuruga mwelekeo wa taifa hilo katika miaka ijayo.
Kwa sasa, dunia inatazama kwa makini kwani wapiganapo simba wawili, nyasi ndizo huumia. Hivyo, katika sakata hili, nyasi ni wananchi na wawekezaji wa Marekani wanaokabiliana na hali ya sintofahamu ya kisiasa na kiuchumi inayozidi kuongezeka siku hadi siku.
REPLY HAPA
image quote pre code