Hali ya Wastara ya Kiafya yazidi kuwa mbaya,tumbo limevimba zaidi
Msanii maarufu wa filamu nchini Tanzania, Wastara Juma, ameibuka kwa mara nyingine akisimulia kwa uchungu mkasa unaoendelea kuutikisa moyo wa mashabiki wake – akidai kuwekwa sumu kwenye soda na mtu anayemhisi ni rafiki wa mdogo wake.
Akiwa kitandani, akiwa na uso wa uchungu na machozi yakimtiririka, Wastara amesema hali yake ya kiafya inazidi kuwa mbaya huku tumbo lake likiwa limevimba vibaya kiasi kwamba linahisi “linataka kupasuka.”
Katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake na kusambaa mitandaoni kupitia chaneli ya Bint Kigoma, Wastara alieleza kuwa mashaka yake makubwa ni kuwa sumu hiyo iliwekwa kimakusudi kwenye soda aliyokunywa, na kwamba mtu aliyefanya hivyo alilenga kumdhuru au hata kumuua.
“Sikutegemea, mtu ambaye nilimwamini kama familia, rafiki wa mdogo wangu, ndiye anayehusishwa na tukio hili. Mange Kimambi anasema watu wanataka nife – mimi sijui kwa nini wanichukie kiasi hiki,” alisema kwa uchungu.
Kwa mujibu wa Wastara, baada ya tukio hilo alianza kuhisi maumivu makali tumboni, hali iliyoambatana na kuvimba kwa tumbo, maumivu ya viungo, na hatimaye kushindwa kabisa kusimama au kufanya kazi zake kama kawaida.
Amewataka Watanzania kumuombea lakini pia kuungana naye katika kutafuta haki kwa kuwa sasa anahitaji msaada mkubwa wa kifedha na matibabu ili kunusuru maisha yake.
“Nimekuwa nikipitia mateso makubwa, nimevumilia kwa muda mrefu lakini sasa naomba msaada. Naomba Serikali, taasisi za haki za binadamu na mashirika ya kupambana na ukatili wanishike mkono. Ninateseka kwa sababu ya wivu wa watu,” alisema kwa sauti ya masikitiko.
Kauli hiyo imeamsha hisia kali mitandaoni ambapo mashabiki, wasanii wenzake, na Watanzania kwa ujumla wameonesha mshikamano mkubwa kwa kumtakia nafuu na kutaka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu madai hayo.
Wapo pia waliotaka jina la mtuhumiwa litajwe hadharani ili sheria ichukue mkondo wake, huku wengine wakitaka vyombo vya usalama kuchunguza tukio hilo ambalo limeonekana kuibua taharuki kubwa katika tasnia ya burudani.
Wastara ameendelea kuwa mmoja wa wasanii waliopitia changamoto nyingi za kiafya na bado kuendelea kuwa na matumaini. Lakini safari hii hali inaonekana kuwa mbaya zaidi, na ujumbe wake kwa taifa ni mmoja tu: “Sitaki huruma, nataka haki.”