Tahadhari ya WHO Kuhusu magonjwa sugu ya kupumua Ulaya

Tahadhari ya WHO Kuhusu magonjwa sugu ya kupumua Ulaya

#1

Tahadhari ya WHO Kuhusu magonjwa sugu ya kupumua Ulaya



Zaidi ya watu milioni 80 wanaishi na magonjwa sugu ya kupumua barani Ulaya, lakini utambuzi hafifu, uchafuzi wa hewa, na kutopewa kipaumbele kisera vinasababisha vifo vinavyoweza kuepukika, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani WHO na Jumuiya ya Madaktari wa Magonjwa ya Mapafu Ulaya (ERS).

Magonjwa sugu ya kupumua (CRDs) kama vile pumu na ugonjwa sugu wa kuzuia hewa ya mapafu (COPD) yanasababisha mamilioni ya vifo kimya kimya kutokana na utambuzi hafifu na kutopewa kipaumbele na sera za afya, imesema ripoti mpya WHO Kanda ya Ulaya na ERS.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 81.7 katika Kanda ya Ulaya ya WHO wanaishi na CRDs, huku milioni 6.8 wakigunduliwa kila mwaka lakini athari halisi ya ugonjwa huu bado haijulikani vizuri kutokana na changamoto katika utambuzi, takwimu, na huduma.

Magonjwa sugu ya kupumua yamesahaulika

Ripoti hii inaonesha kuwa magonjwa sugu ya kupumua yamesahaulika kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa msukumo wa kisera na ufadhili mdogo,” amesema Dkt. Hans Henri P. Kluge, Mkurugenzi wa Kanda ya Ulaya wa WHO. “Kutotekelezwa kwa hatua madhubuti kumesababisha utambuzi hafifu, kutogundulika kwa wakati, na ukosefu wa takwimu sahihi, hali inayogharimu Kanda hii takribani dola bilioni 21 kila mwaka.”

Ameongeza kuwa magonjwa haya ni sababu ya sita inayoongoza kwa vifo katika Kanda hiyo na pia huchangia sana magonjwa ya moyo na saratani.

Changamoto ya ufadhili

Licha ya mafanikio ya awali katika kupunguza vifo vinavyotokana na CRDs, ripoti inaonya kuwa hali hiyo imepelekea kupungua kwa ufadhili wa utafiti na kudhoofika kwa mifumo ya ufuatiliaji.

Aina kuu za magonjwa haya ni COPD na pumu, ambapo COPD inachangia 80% ya vifo vinavyohusiana na CRDs.

Makadirio yanaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wa COPD itaongezeka duniani kwa asilimia 23 kufikia mwaka 2050, huku wanawake na watu wa nchi za kipato cha chini na cha kati wakiwa hatarini zaidi.

Kichocheo cha magonjwa haya
Sababu kuu zinazochochea ongezeko la magonjwa haya ni uvutaji wa tumbaku na uchafuzi wa hewa, ambazo zote zinaweza kuzuiwa.

Ripoti inaonesha kuwa asilimia 25.3 ya watu wazima katika Kanda ya Ulaya bado wanavuta sigara juu ya wastani wa kimataifa.

Wakati huo huo, zaidi ya asilimia 90 ya watu wanapumua hewa chafu yenye chembechembe hatari zinazozidi viwango vya usalama vya WHO.

“Tunakipumua hewa mara 22,000 kwa siku, lakini afya ya upumuaji bado ni eneo linalopuuzwa sana duniani,” amesema Profesa Silke Ryan, Rais wa Jumuiya ya Madaktari wa Magonjwa ya Mapafu Ulaya.

“Ni wakati wa kubadili mtazamo na kuweka afya ya mapafu katika ajenda za sera.”

Athari za kutochukua hatua

Madhara ya kutochukua hatua si ya kiafya tu, bali pia ya kiuchumi na kijamii imesema ripoti hiyo.

Upotevu wa uzalishaji miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 30 hadi 74 kutokana na CRDs unakadiriwa kufikia zaidi ya dola bilioni 20, huku jamii zilizo katika mazingira duni zikikumbwa na athari kubwa zaidi ikiwemo hewa chafu majumbani, maeneo ya kazi yasiyo salama, na ukosefu wa dawa muhimu au gharama kuwa juu mno.

Zaidi ya hayo, bado kuna ukosefu mkubwa wa uwekezaji katika huduma za uboreshaji wa afya, huduma za kupunguza maumivu, na malengo ya afya ya umma yanayopimika.

Wito wa kuchukua hatua

WHO kanda ya Ulaya inatoa wito kwa serikali, jamii za kiraia na sekta ya afya kuchukua hatua sasa, kuelekea Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Mataifa wa 2025 kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs).

“CRDs zimeunganishwa sana na magonjwa mengine kama vile magonjwa ya moyo na saratani ya mapafu,” amesisitiza Dkt. Gauden Galea, Mshauri Mkakati wa WHO barani Ulaya.

“Kwa kutumia maarifa tuliyo nayo, pamoja na mikakati bora iliyothibitishwa, tunaweza kupunguza vifo vinavyotokana na sababu zinazozuilika. Ripoti hii inawapa nchi nyenzo za utekelezaji na uzoefu wa pamoja kusaidia mbinu za afya kwa maisha yote na kujenga Kanda yenye uwezo wa kukabiliana na NCDs na changamoto za afya ya akili ifikapo 2050.”

REPLY HAPA


image quote pre code