Ugonjwa wa Celiac,chanzo,dalili

Ugonjwa wa Celiac,chanzo,dalili

#1

Ugonjwa wa Celiac,chanzo,dalili,Tiba



Ugonjwa wa Celiac ni hali sugu ya kiafya ambapo mfumo wa kinga ya mwili huathiri utumbo mdogo unapokula vyakula vyenye protini inayoitwa gluten. Gluten hupatikana kwenye nafaka kama ngano, shayiri (barley), na rye. Watu wenye ugonjwa huu hawawezi kuvumilia gluten, kwani huanzisha mwitikio wa kinga unaoharibu ukuta wa ndani wa utumbo mdogo na kuathiri ufyonzaji wa virutubisho.

Dalili za Ugonjwa wa Celiac

Dalili za ugonjwa huu hutofautiana kati ya mtu na mtu, na wakati mwingine huonekana taratibu. Baadhi ya watu hawana dalili yoyote, lakini wengine hupata zifuatazo:

Dalili za kawaida kwa watu wazima:

  • Kuharisha mara kwa mara
  • Tumbo kujaa gesi au kuvimba
  • Maumivu ya tumbo
  • Kupungua uzito bila sababu
  • Uchovu ambao hauishi
  • Dalili za upungufu wa madini Chuma mwilini (upungufu wa damu)
  • Ngozi kuwa kavu au vipele (Dermatitis herpetiformis)
  • Dalili za Matatizo ya mifupa (kama Osteoporosis)
  • Kukosa hedhi kwa wanawake

Kwa watoto:

  • Kutokukua vizuri
  • Kuvimba tumbo
  • Kuharisha muda mrefu
  • Pamoja na Dalili zingine za Upungufu wa virutubisho mwilini

Chanzo cha Ugonjwa

Ugonjwa wa Celiac ni ugonjwa wa kinga ya mwili (autoimmune) ambapo mwili hujishambulia wenyewe unapogusana na gluten. Watu wenye historia ya familia ya ugonjwa huu au magonjwa mengine ya kinga (kama kisukari aina ya 1) huwa kwenye hatari kubwa zaidi.

Vipimo na Uchunguzi

Ili kuthibitisha ugonjwa wa Celiac, daktari anaweza kupendekeza:

  1. Vipimo vya damu – kutambua viashiria vya kinga vinavyoashiria mwitikio dhidi ya gluten (kama anti-tTG antibodies).
  2. Biopsy ya utumbo mdogo – kuchukua sampuli ndogo ya tishu ya utumbo ili kuthibitisha uharibifu.

Ni muhimu kufanyiwa vipimo kabla ya kuacha kula vitu vyenye protein ya gluten, au kuanza tiba.

Matibabu

Hakuna tiba ya moja kwa moja ya kuponya ugonjwa wa Celiac, lakini unadhibitiwa kikamilifu kwa:

  • Kufuata mlo usio na gluten maisha yote. Hii ndiyo njia pekee ya kuzuia dalili na kuruhusu utumbo kupona.

  • Kuepuka vyakula vyenye gluten kama:

    • Ngano (wheat)
    • Unga wa ngano
    • Shayiri (barley)
    • Rye
    • Vyakula vya kusindikwa vyenye viambato hivi
  • Kumbuka; Kusoma lebo za vyakula kwa makini kila mara

Baada ya kuanza mlo usio na gluten, dalili nyingi hupungua ndani ya wiki chache hadi miezi kadhaa. Watoto hupona haraka zaidi kuliko watu wazima.

Madhara ya Kutotibu Ugonjwa wa Celiac

Ikiwa haitatibiwa, ugonjwa huu unaweza kusababisha:

  • Upungufu wa virutubisho mwilini
  • Upungufu wa damu sugu
  • Matatizo ya mifupa kama osteopenia au osteoporosis
  • Ugumba au mimba kuharibika
  • Saratani ya utumbo mdogo (kwa nadra sana)

Ushauri wa Lishe

Wasiliana na mtaalamu wa lishe aliyebobea katika lishe isiyo na gluten. Anaweza kukusaidia kupanga mlo bora na kuepuka vyakula hatari.

Vyakula Vinavyoruhusiwa (Gluten-Free Foods)

  • Mchele
  • Viazi
  • Mahindi
  • Mtama (millet)
  • Mboga na matunda yote
  • Pamoja na Vyakula vingine vilivyothibitishwa kutokuwa na gluten

Hitimisho

Ugonjwa wa Celiac ni hali ya kudumu, lakini kwa kuzingatia mlo usio na gluten, watu wengi huishi maisha marefu na yenye afya njema. Uchunguzi wa mapema na elimu kuhusu lishe ni hatua muhimu ya kudhibiti ugonjwa huu.

KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU NA TIBA TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.

Vyanzo vilivyotumika(Sources Used):

  • Mayo Clinic: https://www.mayoclinic.org
  • Cleveland Clinic: https://my.clevelandclinic.org
  • National Institutes of Health (NIH): https://www.niddk.nih.gov

REPLY HAPA


image quote pre code