Utafiti:Ukatili kwa Watoto wenye umri kati ya miaka 13-24 umepungua Tanzania

Utafiti:Ukatili kwa Watoto wenye umri kati ya miaka 13-24 umepungua Tanzania

#1

Utafiti:Ukatili kwa Watoto wenye umri kati ya miaka 13-24 umepungua Tanzania



Matokeo ya utafiti wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na vijana (VACS-2024) yameonyesha ukatili kwa kundi la watoto kati ya miaka 13 hadi 24 umepungua kwa kiwango kikubwa.

Matokeo hayo yameonyesha ukatili wa kingono, kimwili na kihisia kati ya watoto 11,414 umepungua ukilinganisha na utafiti wa kwanza wa VACS-2009 uliofanyika miaka 15 iliyopita.

Akitangaza matokeo hayo leo Jumatatu, Juni 9, 2025 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema utafiti huo uliofanyika kati ya Machi hadi Juni 2024, umeonyesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na utafiti wa awali.

Ametaja kwa watoto wa kike, ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11, ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 76 hadi 24 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 25 hadi 22.

Kwa watoto wa kiume ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia 5, ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi 21 na ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.

"Ninaomba kusisitiza, matokeo haya ya utafiti huu yatawezesha Serikali na wadau kuboresha na kuandaa mipango, programu na mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili nchini itakayoimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana kwa masilahi mapana ya kizazi cha sasa na cha baadaye," amesema Dk Gwajima.

Amesema pamoja na mwenendo huo wa kupungua ukatili, bado Serikali itaendelea kuongeza nguvu zaidi katika kuzuia na kupinga vitendo vya ukatili vinavyojitokeza katika jamii.

Dk Gwajima amesema Serikali itafanya tathmini, mapitio na maboresho ya sera na sheria zilizopo, sambamba na uimarishaji wa programu za kisekta za kuzuia, kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya makundi yote kwa kufanya uchambuzi wa afua zilizoainishwa katika MTAKUWWA  ( Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto) wa pili na kulinganisha na matokeo ya utafiti huu wa pili.

"Hii itasaidia katika kuongeza bajeti na rasilimali watu ili kuzuia ukatili dhidi ya makundi yote na kuboresha huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili," amesema.

Pia ametoa  rai kwa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha ulinzi, usalama wa watoto na vijana unaimarishwa kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii, pamoja na kuendelea kutoa elimu.

Hata hivyo, amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna watoto na vijana wengi wanaoendelea kupitia ukatili wa aina mbalimbali, hivyo ametoa rai ya kuendelea kwa kasi zaidi kuimarisha huduma za kuzuia na kutokomeza ukatili huo pamoja na kuendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto.

Kilichopunguza ukatili

Waziri Gwajima amesema kupungua kwa vitendo vya ukatili huo kunatokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau katika kupinga na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na vijana, kwa kuendelea kutoa elimu mbalimbali kwa umma, pamoja na juhudi za wizara.

"Wizara imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mtoto Sura ya 13 ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake na kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.

"Kutekeleza na kuratibu MTAKUWWA wa awamu ya kwanza na ya pili 2023/24 mpaka 2029/30) ambao unalenga kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili," amesema.

Amesema juhudi za utekelezaji wa programu ya Kitaifa ya Tanzania ya Kizazi Chenye Usawa (2021/2022)  (2025/2026) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa ni miongoni mwa mambo yaliyosaidia.

Amesema kutoa huduma kwa manusura na kuratibu na kusimamia Kampeni ya Taifa ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni (Child Online Protection - COP) katika mikoa ya Tanzania Bara, kampeni iliyolenga kuwaelimisha wazazi, walezi, na watoto kuhusu usalama wa mtoto anapotumia mitandao.

"Kuwezesha wanawake kiuchumi na upatikanaji wa haki, ulinzi na malezi chanya ya watoto na programu zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika nyanja zote za maendeleo imechangia kwa kiasi kikubwa," amesema.

Ametaja programu zingine kuwa ni utoaji wa mafunzo kuhusu sayansi ya malezi, kutoa huduma katika vituo 32 vya mkono kwa mkono (One Stop Centers) na kushughulikia mashauri ya watoto kwa kutumia mfumo wa usimamizi wa mashauri ya watoto NICMS  2017.

Kilichobainika

Akiwasilisha methodolojia ya utafiti huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi za Taifa za Takwimu (NBS) Dk Amina Msengwa amesema utafiti huo uliofanyika kwa watoto kuanzia umri wa miaka 13 hadi 24, ulipita katika kaya 11,414 Tanzania Bara na Visiwani katika mikoa 31.

Amesema utafiti huo ambao umefanyika katika nchi 23, Tanzania imefanya kwa mara ya pili na kuwa miongoni mwa nchi tano pekee zilizofanya kwa mara ya pili.

Dk Msengwa amesema methodolojia waliyoitumia kuna taarifa mpya za kitafiti ambazo zimetumia vifaa vipya vya kimataifa hivyo zinaweza kutumia sehemu yoyote duniani.

"Tumefanya katika maeneo 500, kwenye kaya zipatazo 11,414 hii  inamaanisha kutoka kila kaya tulipata kijana mmoja aliyehojiwa, taarifa nyingi tulizokusanya tulipata umri wa kijana, uzoefu wa ukatili, tabia za kingono, historia na huduma za VVU/Ukimwi na mengineyo mengi," amesema Dk Msengwa.

Akiwasilisha hotuba kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma. Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Zanzibar, Khatib Mwadini Khatib amesema kuna afua nyingi za kiafya ikiwemo za kumlinda mtoto ambazo zimeendelea kufanyika Zanzibar ili kuhakikisha mtoto analindwa.

"Tunahitaji  juhudi za makusudi kupambana na vitendo hivi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha panapojitajika kufanyiwa marekebisho ili kuwakinga na ukatili, tunasimamia na kutekeleza ipasavyo," amesema Khatib.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz amesema usalama wa watoto ni kuhakikisha wanakuwa salama, huru na vitendo vibaya dhidi yao ikiwemo unyanyasaji wa kingono, kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa.

Hata hivyo, Lentz amesema unyanyasaji wa kimwili, kihisia na kingono bado unaendelea kuumiza watoto wengi duniani kote.

Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dk Redempta Mbatia amesema wameshiriki katika utafiti huo kwa kuhakikisha wanaratibu mafunzo kwa wataalamu yaliyotolewa na wakufunzi wa kimataifa kwa kipindi cha mwezi mmoja na wasimamizi wa kazi za kukusanya takwimu.

REPLY HAPA


image quote pre code