DALILI ZA NJIA KUFUNGUKA KWA MJAMZITO
Mwili wa mama mjamzito huanza kujiandaa kwa ajili ya kujifungua siku kadhaa au hata wiki kadhaa kabla ya uchungu halisi kuanza. “njia kufunguka” humaanisha mlango wa kizazi (cervix) kuanza kulegea, kupungua unene na kufunguka ili mtoto aweze kupita wakati wa kujifungua.
Sasa,Je,Zipi ni Dalili zinazoonyesha Njia Kufunguka?
Baadhi ya dalili zinazoweza kuonyesha njia inaanza kufunguka ni hizi:
• Kupata Maumivu ya tumbo yanayokuja na kuondoka kama ya hedhi, lakini yanakuwa ya mara kwa mara na kuongezeka nguvu kadri muda unavyoenda.
• Kupata Maumivu ya mgongo kwa chini, hasa yanayosambaa kuelekea tumboni au mapajani.
• Kutoka ute mzito ukeni wenye rangi ya pinki, kahawia au damu kidogo. Hii huitwa “bloody show” na hutokea baada ya ute uliokuwa umeziba mlango wa kizazi kutoka.
• Kuhisi mtoto kushuka chini zaidi kwenye nyonga. Mama anaweza kupumua vizuri zaidi lakini kwenda chooni mara kwa mara kutokana na presha ya mtoto kushuka.
• Kuhisi presha kubwa sehemu ya nyonga au uke, kana kwamba mtoto anasukuma chini.
• Tumbo kukaza mara kwa mara. Madaktari wanaeleza kuwa uchungu wa kweli huwa haupungui hata ukibadili mkao au kupumzika.
• Maji kutoka ghafla au kuvuja kidogo kidogo. Hii ni dalili muhimu inayoweza kuonyesha uchungu uko karibu au umeanza.
• Baadhi ya wajawazito hupata hali ya kuharisha, uchovu, kutetemeka au kukosa usingizi siku chache kabla ya kujifungua.
KUMBUKA;Wanawake hutofautiana pia,Kwahyo si kila mama hupata dalili zote. Wengine wanaweza kufunguka njia taratibu bila maumivu makali mwanzoni, huku wengine wakianza moja kwa moja na uchungu mkali. Pia wanawake wengine wanaweza kuwa wameanza kufunguka sentimita chache bila hata kujua mpaka Wakapimwa hospitalini.
Uzoefu wa baadhi ya akina mama ulioshirikishwa kwenye majukwaa ya wajawazito unaonyesha kuwa wengine waliona ute wenye damu, maumivu ya mgongo na presha ya nyonga saa au siku chache kabla ya kujifungua, huku wengine wakikaa wiki kadhaa wakiwa wameanza kufunguka njia bila uchungu wa kweli kuanza.
Wataalamu wa afya wanashauri mjamzito kuwahi hospitali haraka ikiwa:
• Uchungu unarudi kila dakika chache na kuongezeka nguvu
• Chupa ya Uzazi imepasuka na Maji yamemwagika(tunaita Ruptured membrane)
• Kuna damu nyingi kutoka ukeni
• Mtoto hapigi mateke au kucheza kama kawaida,na umeona hali hii zaidi ya Saa 24
• Mjamzito Ana dalili za kujifungua kabla ya wiki 37 za ujauzito
Chanzo: Afyaclass,Dr.Ombeni Mkumbwa,Tafiti na maelezo ya wataalamu kutoka Mayo Clinic, Cleveland Clinic, WebMD pamoja na madaktari bingwa wa uzazi duniani.

.jpeg)



Post a Comment
Karibu Afyaclass Bongo Social,Share mawazo yako hapa au chochote kuhusiana na Makala husika,Karibu Sana Mdau Wetu Muhimu.