Hofu Yaongezeka Baada ya Mlipuko wa Hantavirus Kwenye Meli ya Watalii

Mamlaka ya afya nchini Marekani kupitia Centers for Disease Control and Prevention (CDC) inatajwa kutuma maafisa wake kukutana na raia wa Marekani waliopo ndani ya meli ya watalii ya MV Hondius kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa hantavirus ulioripotiwa kuzua taharuki kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na CNN, maafisa hao wanatarajiwa kuifikia meli hiyo katika visiwa vya Canary nchini Hispania kabla ya kupanga usafirishaji wa baadhi ya abiria wa Marekani kwenda jimbo la Nebraska kwa ajili ya hatua za karantini na uchunguzi zaidi wa afya.

Hatua hiyo imekuja baada ya CDC kutoa tahadhari kwa maafisa wa afya katika majimbo ya Texas na New Jersey kuhusu uwezekano wa baadhi ya wakazi kuwa wameathiriwa na virusi hivyo baada ya kuwa kwenye meli hiyo.

Idara ya Afya ya New Jersey imesema watu wawili wanafuatiliwa baada ya kudaiwa kuwa karibu na mtu aliyebainika kuwa na maambukizi ya hantavirus baada ya kushuka kutoka kwenye meli hiyo. Wakati huohuo, maafisa wa afya wa Texas wamesema wakazi wawili wa jimbo hilo waliondoka kwenye meli na kurejea Marekani kabla mamlaka kugundua uwepo wa mlipuko huo.

Hantavirus ni ugonjwa hatari unaohusishwa zaidi na panya na unaweza kuathiri mfumo wa upumuaji wa binadamu. Dalili zake zinaweza kujumuisha homa, uchovu, maumivu ya misuli pamoja na matatizo makubwa ya kupumua endapo hali itazidi kuwa mbaya.

Mpaka sasa, mamlaka za afya zinaendelea kufuatilia hali ya abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo huku uchunguzi zaidi ukiendelea kubaini chanzo na kiwango cha maambukizi.

Tukio hilo limeibua hofu mpya kuhusu usalama wa afya katika safari za meli za watalii huku mamlaka zikisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa haraka na hatua za tahadhari ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi zaidi.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".