Mwezi wa Afya ya Akili: Umuhimu wa Kuzungumza na Kutunza Afya ya Akili

Kila mwezi wa Mei duniani huadhimishwa kama Mwezi wa Uhamasishaji wa Afya ya Akili, kampeni inayolenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili pamoja na kuhamasisha watu kuzungumza wazi kuhusu changamoto za kiakili wanazokutana nazo.

Afya ya akili ni sehemu muhimu ya afya ya jumla ya binadamu kwani inahusisha hali ya kihisia, kisaikolojia pamoja na namna mtu anavyohusiana na jamii inayomzunguka. Pia huathiri jinsi mtu anavyofikiri, kuhisi, kufanya maamuzi na kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha ya kila siku.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Centers for Disease Control and Prevention (CDC), matatizo ya afya ya akili ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoongezeka duniani, huku msongo wa mawazo (depression) na wasiwasi kupita kiasi (anxiety) yakitajwa kuwa matatizo yanayowakumba watu wengi zaidi.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa sababu mbalimbali zinaweza kuchangia kuzorota kwa afya ya akili, ikiwemo umasikini, vitendo vya ukatili, ubaguzi, presha za maisha pamoja na matukio magumu yanayoweza kumuathiri mtu kisaikolojia.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na juhudi kubwa za kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wenye changamoto za afya ya akili, huku mashirika mbalimbali yakihamasisha jamii kutoa msaada na kusikiliza wale wanaopitia changamoto hizo.

Wataalamu wanashauri kuwa kuzungumza na watu wa karibu, kufanya mazoezi, kupata muda wa kupumzika pamoja na kutafuta msaada wa kitaalamu mapema ni baadhi ya njia zinazoweza kusaidia kulinda afya ya akili.

Maadhimisho ya mwaka huu pia yanatoa wito kwa jamii kutambua kuwa afya ya akili ni muhimu sawa na afya ya mwili, na kila mtu ana jukumu la kusaidia kujenga mazingira salama na yenye msaada kwa wote.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".