Vipimo vya DNA vyasababisha mwanamke mmoja kulipa $2,500

Mahakama moja mjini Hwange nchini Zimbabwe  imemwamuru mwanamke kurejesha dola za Marekani 2,500 baada ya vipimo vya DNA kubaini kuwa mwanaume aliyekuwa akitoa matunzo ya mtoto kwa miaka kadhaa hakuwa baba halali wa mtoto huyo.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya mgogoro wa muda mrefu wa ubaba uliomhusisha mwanaume aitwaye Clean Nyathi ambaye alisema alianza kuwa na mashaka kuhusu uhalali wa mtoto tangu mwaka 2014 na mara kadhaa aliomba kufanyika kwa vipimo vya DNA.

Nyathi alisema tangu mwanzo alikuwa akihisi mtoto huyo si wake jambo lililomfanya kuendelea kusisitiza kupimwa DNA ili kupata ukweli. Alidai aliyekuwa mwenza wake Cynthia Dube alikuwa akikataa mara kwa mara kufanya vipimo hivyo hali iliyoongeza mashaka kwake.

Kwa mujibu wa Nyathi, baada ya kusubiri kwa muda mrefu alilazimika kugharamia mwenyewe vipimo vya DNA kwa takribani dola 450 za Marekani. Matokeo ya vipimo hivyo yalionyesha kuwa baba halisi wa mtoto alikuwa mwanaume mwingine.

Kabla ya matokeo hayo kutoka, Nyathi alikuwa tayari amelipa matunzo ya mtoto kwa miaka kadhaa. Alisema kiwango cha fedha alichokuwa akitoa kilianza kwa dola 40 kabla ya kuongezeka hadi dola 50 na baadaye dola 60 kwa mwezi huku akiendelea kuamini analea mtoto wake wa damu.

Baada ya matokeo ya DNA kuthibitisha ukweli huo, mahakama iliamuru Dube kurejesha dola 2,500 ndani ya siku saba. Hata hivyo, mwanamke huyo alidai hana uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha ndani ya muda uliowekwa.

Dube alieleza kuwa alimfahamu Nyathi wakati tayari akiwa kwenye uhusiano mwingine na baadaye akaanza kuishi naye baada ya matatizo katika mahusiano yake ya awali. Pia alidai alikuwa tayari mjamzito kabla ya kuhamia kwa Nyathi jambo lililosababisha mvutano wa muda mrefu kuhusu suala la matunzo ya mtoto.

Aidha alisema ingawa baadaye alikubali kufanyika kwa vipimo vya DNA, ucheleweshaji wa mchakato huo uliufanya mgogoro huo kudumu kwa miaka kadhaa zaidi.

Kwa sasa Nyathi amesema hajaanza hatua za haraka za kutekeleza amri ya mahakama lakini ameonya kuwa yuko tayari kurejea mahakamani iwapo fedha hizo hazitarejeshwa kama ilivyoamriwa.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".