Matatizo ya Ulaji Wakati wa Ujauzito,Hatari Inayopuuzwa Lakini Inaweza Kutibika
Ujauzito huleta mabadiliko mengi ya mwili na hisia kwa mwanamke. Homoni hubadilika, tumbo hukua, na uzito huongezeka ili kuweza kumlea mtoto anayekua tumboni. Kwa wanawake wengi, mabadiliko haya ni sehemu ya kawaida ya safari ya ujauzito. Hata hivyo, kwa baadhi ya wanawake, hasa wale wenye historia ya matatizo ya ulaji kama anorexia au bulimia, kipindi hiki kinaweza kuwa changamoto kubwa ya afya ya akili.
Mtafiti na mhadhiri wa afya ya umma, Elizabeth Claydon, anasimulia kuwa alipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 27 wakati bado alikuwa katika hatua za kupona kutokana na anorexia. Kadri mwili wake ulivyobadilika kwa kasi kutokana na ujauzito, mawazo ya ugonjwa huo yalirejea kwa nguvu.
"Baadhi ya siku nilikubaliana na mabadiliko ya mwili wangu, lakini siku nyingine ilikuwa vigumu sana. Nilipojiangalia kwenye kioo nilihisi kama simtambui mtu ninayemwona," anasema Claydon.
Anorexia nervosa ni ugonjwa unaomfanya mtu kuwa na hofu kubwa ya kuongezeka uzito na mara nyingi husababisha kula chakula kidogo sana. Claydon alikuwa ameugua ugonjwa huo tangu akiwa na miaka 16 na alifanikiwa kupona akiwa na miaka 22. Hata hivyo, alirejea kwenye dalili za tatizo hilo akiwa na miaka 26, muda mfupi kabla ya kupata ujauzito.
Wataalamu wanasema hali kama hii si ya kawaida sana, lakini pia si nadra kama watu wengi wanavyodhani. Tafiti zinaonyesha kuwa takribani mwanamke mmoja kati ya 20 hupata tatizo la ulaji wakati wa ujauzito. Baadhi yao huwa na historia ya matatizo hayo na hupata kurejea kwenye dalili hizi tena, huku wengine wakianza kuonyesha dalili kwa mara ya kwanza wanapokuwa wajawazito.
Tatizo hili linaweza kuleta madhara makubwa kwa mama na mtoto. Lishe duni wakati wa ujauzito inaweza kuongeza hatari ya mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, kuzaliwa kabla ya wakati, au kupata matatizo ya ukuaji. Kwa upande wa mama, kunaweza kutokea upungufu wa virutubisho muhimu, uchovu mkubwa, matatizo ya afya ya akili na hata ugumu wa kujenga uhusiano wa karibu na mtoto baada ya kujifungua.
Changamoto nyingine ni kwamba matatizo haya mara nyingi hayagunduliwi mapema katika mfumo wa huduma za afya. Wajawazito wengi wenye dalili za matatizo ya ulaji huweza kuficha hali yao au kutotambua kuwa wanahitaji msaada wa kitaalamu.
Hata hivyo, watafiti wanaamini kuwa ujauzito unaweza pia kuwa fursa muhimu ya kupona. Kwa wanawake wengi, hamu ya kumlinda mtoto wao huwapa motisha ya kutafuta matibabu, kuboresha ulaji wao na kujenga uhusiano mzuri zaidi na miili yao.
Wataalamu wanashauri wanawake wajawazito wanaopambana na hofu kali ya kuongezeka uzito, kula kwa kiwango kidogo sana, au mawazo ya mara kwa mara kuhusu umbo la mwili wao kuzungumza na daktari, mtaalamu wa lishe au mtaalamu wa afya ya akili mapema iwezekanavyo. Matibabu ya mapema yanaweza kusaidia kulinda afya ya mama na mtoto kwa wakati mmoja.
Chanzo: Makala ya BBC Future kuhusu matatizo ya ulaji wakati wa ujauzito na uzoefu wa Elizabeth Claydon.



Post a Comment