Showing posts with label Ripoti ya WHO. Show all posts
Showing posts with label Ripoti ya WHO. Show all posts

Wagonjwa wa Malaria waliongezeka duniani 2024,WHOAfyaclass Forum •

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema ugonjwa wa malaria uliwaua takribani watu 610,000 duniani kote mwaka 2024.


Ripoti ya mwaka ya WHO kuhusu malaria iliyotolewa Alhamisi, imeeleza kuwa visa vya ugonjwa huo vimeongezeka zaidi nchini Ethiopia, Madagascar na Yemen.

Idadi hiyo ni juu kidogo ikilinganishwa na vifo vya 2023, huku maambukizi mapya yakipanda kutoka milioni 273 hadi takribani milioni 282.

Baada ya hatua kubwa kupigwa mwanzoni mwa miaka ya 2000, mapambano dhidi ya malaria yamekuwa yakisuasua katika muongo mmoja uliopita.

Nchi kadhaa hazina malaria

Hata hivyo, nchi 47 zimethibitishwa kutokuwa na malaria.

Daniel Ngamije Madandi, Mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa wa Kupambana na Malaria wa WHO, amesema watu wengi bado wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa ambao unaweza kuzuilika na kutibika.

WHO imesema kuongezeka kwa maambukizi kunachangiwa na ongezeko la dawa zisizo na ubora wa kutibu malaria, mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa ufadhili.

0 Comment

Chanjo mpya za TB zina uwezo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa haraka 'WHO'Afyaclass Forum •

Ripoti:WHO yahimiza hatua thabiti kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo mpya za TB

WHO inasisitiza umuhimu wa utafiti kuhusu ugonjwa wa Kifua kikuu hasa kile kilicho sugu dhidi ya dawa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua ripoti mpya leo pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Afya wa G20 uliofanyika Limpopo, Afrika Kusini, likitoa wito kwa hatua thabiti za kifedha na upatikanaji ili kuhakikisha chanjo mpya za kifua kikuu  (TB) zinawafikia vijana balehe na watu wazima katika nchi zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo.

Ripoti hiyo, yenye kichwa, “kuchochea suluhisho kwa upatikanaji sawa duniani na ufadhili endelevu wa chanjo mpya za kifua kikuu kwa watu wazima na vijana,” imetoa uchambuzi wa kwanza wa aina yake kuhusu vikwazo vinavyotarajiwa, vizuizi, na mienendo ya soko ambayo inaweza kuathiri upatikanaji wa wakati, usawa, na endelevu wa chanjo mpya za TB.

“Chanjo mpya za TB zina uwezo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa haraka na kubadilisha mwelekeo wa janga hili, kwa kutumia nguvu ya sayansi, ushirikiano na fedha, tunaweza kufanikisha maono yetu ya pamoja ya kutokomeza kifua kikuu.”  amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

0 Comment

WHO:Magonjwa ya neva hukatili Maisha ya watu milioni 11 kila mwakaAfyaclass Forum •

Magonjwa ya neva hukatili Maisha ya watu milioni 11 kila mwaka: WHO



Shirika la Afya Duniani (WHO) leo limetoa onyo kwamba magonjwa ya ubongo husababisha vifo zaidi ya milioni 11 kila mwaka duniani, yakigusa zaidi ya asilimia 40 ya idadi ya watu duniani ambao ni zaidi ya watu bilioni 3.

Kwenye Ripoti ya Hali ya Neva Duniani iliyotolewa leo mjini Geneva na Seoul na WHO, inaonesha kwamba chini ya nchi 1 kati ya 1 ina sera ya kitaifa ya kushughulikia ongezeko la mzigo wa magonjwa haya, ambayo ni pamoja na kiharusi, ugonjwa wa kusahau, maumivu ya Kichwa ya muda mrefu, kifafa na saratani za mfumo wa neva.

Tofauti za huduma kwenye nchi mbalimbali

Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi zenye kipato cha chini zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa ubongo, baadhi zikiwa na mara 82 chini ya idadi ya wananolojia kwa kila 100,000 ikilinganishwa na nchi zenye kipato cha juu.

Licha ya ongezeko la magonjwa ya ubongo, nchi nyingi hazina mipango ya kitaifa, ufadhili maalum, na wafanyakazi wa kutosha katika huduma za afya.

WHO inasisitiza kuwa hatua za dharura, zinazoratibiwa vizuri zinahitajika kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza tofauti za kiafya.

Mapengo makubwa katika huduma na bima ya afya

Ripoti inaonesha kuwa nchi 25 tu zinajumuisha magonjwa ya ubongo kwenye bima zao za afya za msingi.

Huduma muhimu kama vile vitengo vya kiharusi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya neva, tiba ya kurejea afya, na huduma za kumaliza maumivu, mara nyingi zipo mijini, na kuacha wananchi wa vijijini na maeneo yenye ukosefu wa huduma bila msaada muhimu wa kuokoa maisha.

Kampeni za uhamasishaji na utetezi wa umma bado ni chache, zikiacha wagonjwa na familia wakikabili unyanyapaa na ubaguzi wa kijamii.

Watoa huduma wamesahaulika

WHO inasema magonjwa ya ubongo mara nyingi yanahitaji huduma ya maisha yote, lakini nchi 46 tu zinatoa huduma rasmi kwa wale wanaowahudumia wagonjwa, na nchi 44 tu zina ulinzi wa kisheria kwa wanaojitolea.

Ripoti inasema wanaojitolea kutoa huduma, wengi wao ni wanawake, na wanakabiliwa na mzigo wa kifedha na ukosefu wa haki za kijamii.

WHO imesisitiza kuwa bila kutambuliwa na kuungwa mkono ipasavyo, familia zinabaki kubeba mzigo mkubwa, zikiongeza pengo la kiafya duniani.

WHO yataka hatua za kimataifa

Kuhusu hili, WHO imezihimiza serikali kufanya magonjwa ya ubongo kuwa kipaumbele cha sera, kupanua upatikanaji wa huduma kupitia bima ya afya ya msingi, kukuza afya ya ubongo katika mzunguko mzima wa maisha, na kuimarisha mifumo ya takwimu kwa maamuzi yanayotegemea ushahidi.

Nchi Wanachama walikubali Mpango wa Kimataifa wa Kila Sekta juu ya kifafa na magonjwa mengine ya ubongo mwaka 2022, lakini utekelezaji bado haujafikia kiwango kinachotakiwa na upungufu wa ufadhili unaendelea.

Njia za kuziba pengo la afya duniani

Dkt. Jeremy Farrar, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO, amesema “Magonjwa mengi ya ubongo yanaweza kuzuiwa au kutibiwa kwa ufanisi, lakini huduma bado hazipatikani kwa wengi hasa katika maeneo ya vijijini na maeneo yasiyo na huduma za afya.”

Ameongeza kuwa Lazima tufanye kazi pamoja kuhakikisha wagonjwa na familia zao wanapewa kipaumbele na afya ya ubongo inafadhiliwa ipasavyo.”

Bila hatua thabiti, WHO inasema, magonjwa ya ubongo yataendelea kuongezeka, na kuongeza tofauti za kiafya duniani. UN

0 Comment

Shinikizo la damu kuwaweka hatarini watu zaidi ya bilioni moja duniani – Ripoti ya WHOAfyaclass Forum •

Shinikizo la damu lisilodhibitiwa lawaweka hatarini watu zaidi ya bilioni moja duniani – Ripoti ya WHO



Dk. Shuaib anaangalia shinikizo la damu na kutoa nyenzo za elimu kwa wanawake wakati wa kampeni ya uhamasishaji dhidi ya ukeketaji wa wanawake (FGM) katika kambi ya Rabbi Yasir kwa wakimbizi wa ndani nje kidogo ya Mogadishu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limezindua ripoti yake ya pili ya kimataifa kuhusu shinikizo la damu, ikionesha kuwa watu bilioni 1.4 waliishi na tatizo hilo mnamo mwaka 2024. Hata hivyo, ni zaidi kidogo ya mtu mmoja kati ya watano walioweza kulidhibiti kupitia dawa au kubadili mitindo ya maisha yenye hatari kiafya.

Ripoti hiyo mpya imezinduliwa leo  Jumanne,tarehe 23 mwezi Septemba 2025 wakati wa hafla iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya WHO na taasisi kama Bloomberg Philanthropies na Resolve to Save Lives wakati wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Pia ripoti imebaini kuwa ni asilimia 28 pekee ya nchi zenye kipato cha chini zinazoripoti upatikanaji wa dawa zote zinazopendekezwa na WHO katika maduka ya dawa au vituo vya afya vya msingi.

Shinikizo la damu ni nini?

Shinikizo la damu ni moja ya visababishi vikuu vya mshtuko wa moyo, kiharusi, ugonjwa sugu wa figo na hata shida ya kupoteza kumbukumbu. Ni tatizo linaloweza kuzuilika na kutibika, lakini bila hatua za haraka, mamilioni wataendelea kufariki mapema huku nchi zikikabiliwa na hasara kubwa za kiuchumi. Kuanzia mwaka 2011 hadi 2025, magonjwa ya moyo na mishipa—yakiwemo shinikizo la damu—yanakadiriwa kugharimu nchi zenye kipato cha chini na cha kati kiasi cha dola trilioni 3.7 za Kimarekani, sawa na takribani  asilimia 2 ya jumla ya pato lao la taifa.

Kwa kila saa moja, maisha zaidi ya 1,000 yanapotea kutokana na kiharusi na mshtuko wa moyo unaosababishwa na shinikizo la damu, na vifo vingi kati ya hivyo vinaweza kuzuilika,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.

Ameongeza Dr. Tedros “Nchi zina nyenzo za kubadili hali hii. Kwa dhamira ya kisiasa, uwekezaji endelevu na mabadiliko ya mifumo ya huduma za afya ili kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu, tunaweza kuokoa mamilioni ya maisha na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.”

Kwa mujibu wa Dkt. Kelly Henning, kiongozi wa mpango wa afya ya umma wa Bloomberg Philanthropies: “Shinikizo la damu lisilodhibitiwa husababisha idadi ya vifo zaidi ya milioni 10 kila mwaka, licha ya kuwa ni tatizo linaloweza kuzuilika na kutibika. Nchi zinazojumuisha huduma za shinikizo la damu katika bima ya afya kwa wote na huduma za msingi zinafanya maendeleo makubwa, lakini nchi nyingi zenye kipato cha chini na cha kati bado zimesalia nyuma. Sera madhubuti za kuongeza uelewa na upatikanaji wa matibabu ni muhimu ili kupunguza maradhi ya moyo na vifo vinavyoweza kuzuilika.”

Vikwazo vinavyoendelea

Takwimu kutoka nchi na maeneo 195 zinaonesha kuwa nchi 99 zina viwango vya udhibiti wa shinikizo la damu chini ya asilimia 20. Wengi wa waathirika wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambako mifumo ya afya ina changamoto za rasilimali.

Ripoti imeweka wazi mapengo makubwa katika kinga, uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa muda mrefu. Vikwazo vikuu ni pamoja na sera dhaifu za afya ya umma dhidi ya hatari kama vile matumizi ya pombe na tumbaku, kutofanya mazoezi, ulaji mwingi wa chumvi na mafuta yenye madhara; ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kupima shinikizo la damu; uhaba wa miongozo ya matibabu na timu za afya ya msingi zilizo na ujuzi; upungufu wa mnyororo wa ugavi na gharama kubwa za dawa; ukosefu wa kinga ya kifedha kwa wagonjwa; pamoja na mifumo dhaifu ya taarifa za ufuatiliaji.

Upatikanaji wa dawa – nguzo ya mafanikio

Dawa za shinikizo la damu ni miongoni mwa nyenzo bora zaidi na nafuu za afya ya umma. Hata hivyo, nchi 7 kati ya 25 zenye kipato cha chini (sawa na asilimia 28) ndizo pekee zinaripoti kuwa dawa zote zinazopendekezwa na WHO zinapatikana kwa ujumla, ikilinganishwa na asilimia 93 ya nchi zenye kipato cha juu.

Dawa salama, bora na za gharama nafuu za kudhibiti shinikizo la damu zipo, lakini bado watu wengi sana hawazipati,” amesema Dkt. Tom Frieden, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Resolve to Save Lives. “Kuziba pengo hili kutaokoa maisha na pia kuokoa mabilioni ya dola kila mwaka.”

Mafanikio katika nchi mbalimbali licha ya changamoto

Licha ya changamoto, baadhi ya nchi zimeonesha mafanikio makubwa kwa kuingiza huduma za shinikizo la damu katika bima ya afya kwa wote, kuimarisha huduma za msingi na kushirikisha jamii:

Bangladesh: imeongeza udhibiti wa shinikizo la damu kutoka asilimia 15 hadi asilimia 56 katika baadhi ya maeneo kati ya mwaka 2019 na 2025 kwa kujumuisha huduma hizo katika kifurushi cha huduma muhimu za afya na kuimarisha uchunguzi na ufuatiliaji.

Ufilipino: umejumuisha ipasavyo kifurushi cha kiufundi cha WHO kinachoitwa HEARTS katika huduma za kijamii kote nchini.

Korea Kusini: imefanya mageuzi ya kiafya kwa kupunguza gharama za dawa za shinikizo la damu na ada za wagonjwa, na kufanikisha viwango vya juu vya udhibiti wa shinikizo la damu kitaifa – asilimia 59 mwaka 2022.

WHO imetoa wito kwa nchi zote kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu katika mageuzi ya huduma za afya kwa wote. Utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti unaweza kuzuia mamilioni ya vifo vya mapema na kupunguza gharama kubwa za kijamii na kiuchumi zinazotokana na tatizo hili.

0 Comment
Notification
My blog is in the process of editing and perfecting the new template, so there are still some functions to click but not yet used. Note which blogs associated with your side please read this lesson to update the blog logo.
UNDERSTOOD