Shinikizo la damu lisilodhibitiwa lawaweka hatarini watu zaidi ya bilioni moja duniani – Ripoti ya WHO
Dk. Shuaib anaangalia shinikizo la damu na kutoa nyenzo za elimu kwa wanawake wakati wa kampeni ya uhamasishaji dhidi ya ukeketaji wa wanawake (FGM) katika kambi ya Rabbi Yasir kwa wakimbizi wa ndani nje kidogo ya Mogadishu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limezindua ripoti yake ya pili ya kimataifa kuhusu shinikizo la damu, ikionesha kuwa watu bilioni 1.4 waliishi na tatizo hilo mnamo mwaka 2024. Hata hivyo, ni zaidi kidogo ya mtu mmoja kati ya watano walioweza kulidhibiti kupitia dawa au kubadili mitindo ya maisha yenye hatari kiafya.
Ripoti hiyo mpya imezinduliwa leo Jumanne,tarehe 23 mwezi Septemba 2025 wakati wa hafla iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya WHO na taasisi kama Bloomberg Philanthropies na Resolve to Save Lives wakati wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Pia ripoti imebaini kuwa ni asilimia 28 pekee ya nchi zenye kipato cha chini zinazoripoti upatikanaji wa dawa zote zinazopendekezwa na WHO katika maduka ya dawa au vituo vya afya vya msingi.
Shinikizo la damu ni nini?
Shinikizo la damu ni moja ya visababishi vikuu vya mshtuko wa moyo, kiharusi, ugonjwa sugu wa figo na hata shida ya kupoteza kumbukumbu. Ni tatizo linaloweza kuzuilika na kutibika, lakini bila hatua za haraka, mamilioni wataendelea kufariki mapema huku nchi zikikabiliwa na hasara kubwa za kiuchumi. Kuanzia mwaka 2011 hadi 2025, magonjwa ya moyo na mishipa—yakiwemo shinikizo la damu—yanakadiriwa kugharimu nchi zenye kipato cha chini na cha kati kiasi cha dola trilioni 3.7 za Kimarekani, sawa na takribani asilimia 2 ya jumla ya pato lao la taifa.
“Kwa kila saa moja, maisha zaidi ya 1,000 yanapotea kutokana na kiharusi na mshtuko wa moyo unaosababishwa na shinikizo la damu, na vifo vingi kati ya hivyo vinaweza kuzuilika,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.
Ameongeza Dr. Tedros “Nchi zina nyenzo za kubadili hali hii. Kwa dhamira ya kisiasa, uwekezaji endelevu na mabadiliko ya mifumo ya huduma za afya ili kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu, tunaweza kuokoa mamilioni ya maisha na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.”
Kwa mujibu wa Dkt. Kelly Henning, kiongozi wa mpango wa afya ya umma wa Bloomberg Philanthropies: “Shinikizo la damu lisilodhibitiwa husababisha idadi ya vifo zaidi ya milioni 10 kila mwaka, licha ya kuwa ni tatizo linaloweza kuzuilika na kutibika. Nchi zinazojumuisha huduma za shinikizo la damu katika bima ya afya kwa wote na huduma za msingi zinafanya maendeleo makubwa, lakini nchi nyingi zenye kipato cha chini na cha kati bado zimesalia nyuma. Sera madhubuti za kuongeza uelewa na upatikanaji wa matibabu ni muhimu ili kupunguza maradhi ya moyo na vifo vinavyoweza kuzuilika.”
Vikwazo vinavyoendelea
Takwimu kutoka nchi na maeneo 195 zinaonesha kuwa nchi 99 zina viwango vya udhibiti wa shinikizo la damu chini ya asilimia 20. Wengi wa waathirika wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambako mifumo ya afya ina changamoto za rasilimali.
Ripoti imeweka wazi mapengo makubwa katika kinga, uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa muda mrefu. Vikwazo vikuu ni pamoja na sera dhaifu za afya ya umma dhidi ya hatari kama vile matumizi ya pombe na tumbaku, kutofanya mazoezi, ulaji mwingi wa chumvi na mafuta yenye madhara; ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kupima shinikizo la damu; uhaba wa miongozo ya matibabu na timu za afya ya msingi zilizo na ujuzi; upungufu wa mnyororo wa ugavi na gharama kubwa za dawa; ukosefu wa kinga ya kifedha kwa wagonjwa; pamoja na mifumo dhaifu ya taarifa za ufuatiliaji.
Upatikanaji wa dawa – nguzo ya mafanikio
Dawa za shinikizo la damu ni miongoni mwa nyenzo bora zaidi na nafuu za afya ya umma. Hata hivyo, nchi 7 kati ya 25 zenye kipato cha chini (sawa na asilimia 28) ndizo pekee zinaripoti kuwa dawa zote zinazopendekezwa na WHO zinapatikana kwa ujumla, ikilinganishwa na asilimia 93 ya nchi zenye kipato cha juu.
“Dawa salama, bora na za gharama nafuu za kudhibiti shinikizo la damu zipo, lakini bado watu wengi sana hawazipati,” amesema Dkt. Tom Frieden, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Resolve to Save Lives. “Kuziba pengo hili kutaokoa maisha na pia kuokoa mabilioni ya dola kila mwaka.”
Mafanikio katika nchi mbalimbali licha ya changamoto
Licha ya changamoto, baadhi ya nchi zimeonesha mafanikio makubwa kwa kuingiza huduma za shinikizo la damu katika bima ya afya kwa wote, kuimarisha huduma za msingi na kushirikisha jamii:
Bangladesh: imeongeza udhibiti wa shinikizo la damu kutoka asilimia 15 hadi asilimia 56 katika baadhi ya maeneo kati ya mwaka 2019 na 2025 kwa kujumuisha huduma hizo katika kifurushi cha huduma muhimu za afya na kuimarisha uchunguzi na ufuatiliaji.
Ufilipino: umejumuisha ipasavyo kifurushi cha kiufundi cha WHO kinachoitwa HEARTS katika huduma za kijamii kote nchini.
Korea Kusini: imefanya mageuzi ya kiafya kwa kupunguza gharama za dawa za shinikizo la damu na ada za wagonjwa, na kufanikisha viwango vya juu vya udhibiti wa shinikizo la damu kitaifa – asilimia 59 mwaka 2022.
WHO imetoa wito kwa nchi zote kujumuisha udhibiti wa shinikizo la damu katika mageuzi ya huduma za afya kwa wote. Utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti unaweza kuzuia mamilioni ya vifo vya mapema na kupunguza gharama kubwa za kijamii na kiuchumi zinazotokana na tatizo hili.
image quote pre code