Magonjwa ya neva hukatili Maisha ya watu milioni 11 kila mwaka: WHO
Shirika la Afya Duniani (WHO) leo limetoa onyo kwamba magonjwa ya ubongo husababisha vifo zaidi ya milioni 11 kila mwaka duniani, yakigusa zaidi ya asilimia 40 ya idadi ya watu duniani ambao ni zaidi ya watu bilioni 3.
Kwenye Ripoti ya Hali ya Neva Duniani iliyotolewa leo mjini Geneva na Seoul na WHO, inaonesha kwamba chini ya nchi 1 kati ya 1 ina sera ya kitaifa ya kushughulikia ongezeko la mzigo wa magonjwa haya, ambayo ni pamoja na kiharusi, ugonjwa wa kusahau, maumivu ya Kichwa ya muda mrefu, kifafa na saratani za mfumo wa neva.
Tofauti za huduma kwenye nchi mbalimbali
Kwa mujibu wa ripoti hiyo nchi zenye kipato cha chini zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa ubongo, baadhi zikiwa na mara 82 chini ya idadi ya wananolojia kwa kila 100,000 ikilinganishwa na nchi zenye kipato cha juu.
Licha ya ongezeko la magonjwa ya ubongo, nchi nyingi hazina mipango ya kitaifa, ufadhili maalum, na wafanyakazi wa kutosha katika huduma za afya.
WHO inasisitiza kuwa hatua za dharura, zinazoratibiwa vizuri zinahitajika kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza tofauti za kiafya.
Mapengo makubwa katika huduma na bima ya afya
Ripoti inaonesha kuwa nchi 25 tu zinajumuisha magonjwa ya ubongo kwenye bima zao za afya za msingi.
Huduma muhimu kama vile vitengo vya kiharusi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya neva, tiba ya kurejea afya, na huduma za kumaliza maumivu, mara nyingi zipo mijini, na kuacha wananchi wa vijijini na maeneo yenye ukosefu wa huduma bila msaada muhimu wa kuokoa maisha.
Kampeni za uhamasishaji na utetezi wa umma bado ni chache, zikiacha wagonjwa na familia wakikabili unyanyapaa na ubaguzi wa kijamii.
Watoa huduma wamesahaulika
WHO inasema magonjwa ya ubongo mara nyingi yanahitaji huduma ya maisha yote, lakini nchi 46 tu zinatoa huduma rasmi kwa wale wanaowahudumia wagonjwa, na nchi 44 tu zina ulinzi wa kisheria kwa wanaojitolea.
Ripoti inasema wanaojitolea kutoa huduma, wengi wao ni wanawake, na wanakabiliwa na mzigo wa kifedha na ukosefu wa haki za kijamii.
WHO imesisitiza kuwa bila kutambuliwa na kuungwa mkono ipasavyo, familia zinabaki kubeba mzigo mkubwa, zikiongeza pengo la kiafya duniani.
WHO yataka hatua za kimataifa
Kuhusu hili, WHO imezihimiza serikali kufanya magonjwa ya ubongo kuwa kipaumbele cha sera, kupanua upatikanaji wa huduma kupitia bima ya afya ya msingi, kukuza afya ya ubongo katika mzunguko mzima wa maisha, na kuimarisha mifumo ya takwimu kwa maamuzi yanayotegemea ushahidi.
Nchi Wanachama walikubali Mpango wa Kimataifa wa Kila Sekta juu ya kifafa na magonjwa mengine ya ubongo mwaka 2022, lakini utekelezaji bado haujafikia kiwango kinachotakiwa na upungufu wa ufadhili unaendelea.
Njia za kuziba pengo la afya duniani
Dkt. Jeremy Farrar, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO, amesema “Magonjwa mengi ya ubongo yanaweza kuzuiwa au kutibiwa kwa ufanisi, lakini huduma bado hazipatikani kwa wengi hasa katika maeneo ya vijijini na maeneo yasiyo na huduma za afya.”
Ameongeza kuwa Lazima tufanye kazi pamoja kuhakikisha wagonjwa na familia zao wanapewa kipaumbele na afya ya ubongo inafadhiliwa ipasavyo.”
Bila hatua thabiti, WHO inasema, magonjwa ya ubongo yataendelea kuongezeka, na kuongeza tofauti za kiafya duniani. UN
image quote pre code