Milio ya Risasi Yarindima Nje ya Nyumba ya Chris Brown Los Angeles
Hali ya taharuki ilitawala eneo la Tarzana, jijini Los Angeles, baada ya milio ya risasi kusikika nje ya nyumba ya msanii maarufu Chris Brown, tukio lililotokea mchana wa Ijumaa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyombo vya usalama, polisi walipokea simu majira ya saa kumi jioni zikieleza uwepo wa tukio la ufyatuaji risasi katika eneo hilo. Mwanamke mmoja alidai kuwa mwanaume alimfyatulia risasi kwenye gari lake kufuatia mzozo uliotokea kati yao.
Inaelezwa kuwa mtuhumiwa alitambulika kama mwanaume mweusi mwenye umri wa takriban miaka 35. Askari walipowasili eneo la tukio, waliwakuta watu wote wawili waliokuwa wakihusika na tukio hilo na kuanza kuwahoji ili kubaini kilichotokea.
Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya mtuhumiwa, mzozo huo ulianza baada ya mwanamke huyo kukataa kuondoka eneo hilo, hali iliyosababisha mabishano makali. Tukio hilo lilizidi kuwa baya pale ambapo mwanamke huyo alidaiwa kuendesha gari lake na kumpita juu ya mguu mtuhumiwa, jambo lililomfanya ajibu kwa kufyatua risasi kuelekea kwenye gari hilo.
Baada ya tukio hilo, polisi walimkamata mtuhumiwa papo hapo na kumchukulia hatua za kisheria kwa tuhuma za kutumia silaha hatari pamoja na uharibifu wa mali.
Maafisa wa usalama walisisitiza kuwa tukio hilo halikutokea ndani ya nyumba ya Chris Brown bali nje, barabarani karibu na makazi yake. Hadi sasa, haijathibitishwa kama msanii huyo alikuwa nyumbani wakati wa tukio hilo au kama wahusika walikuwa na uhusiano wowote naye.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea huku mamlaka zikichukua hatua kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa katika eneo hilo.





Post a Comment
WEKA MAONI HAPA(Reply)