Maelfu ya familia katika Kaunti ya Garissa nchini Kenya zimelazimika kuyahama makazi yao kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji katika Mto Tana.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Garissa County Steering Group, zaidi ya kaya 10,000 katika eneo la Garissa Township tayari zimeathirika na kuondolewa makwao, huku zaidi ya kaya 60,000 kote kauntini humo zikiwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko hayo ambayo yanaendelea kuongezeka siku hadi siku.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na vijiji vya Bulla Punda, Bulla Kamor, Bulla Sheikh, Bakuyu na Ziwani, ambapo wananchi wengi wamelazimika kuyaacha makazi yao baada ya nyumba kufunikwa na maji. Mashamba, mifugo pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi zimeharibiwa vibaya, hali inayozidi kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa maeneo hayo.
Familia zilizopoteza makazi kwa sasa zimehifadhiwa katika kambi za muda zikiwemo Farmers Training Centre (FTC), Hyuga pamoja na Police Training Centres huku serikali za mitaa na mashirika ya kibinadamu zikiendelea kutoa msaada wa dharura kwa waathirika.
Wananchi katika maeneo hayo wameendelea kuiomba serikali kuongeza juhudi za uokoaji na misaada ya kibinadamu, wakihofia kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi ikiwa mvua zitaendelea kunyesha katika siku zijazo.





Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".