Afrika Kusini kunufaika na chanjo mpya ya kupambana na VVU

Afrika Kusini kunufaika na chanjo mpya ya kupambana na VVU

#1

Afrika Kusini taifa lenye idadi kubwa zaidi duniani ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI limeingia kwenye orodha ya nchi za kwanza kunufaika na chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi, iitwayo Lenacapavir.

Chanjo hii itakayoleta mapinduzi katika sekta ya afya, inawalenga watu ambao bado hawajaambukizwa, lakini wako katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Kupitia dawa hii, mtu atahitaji kuchoma sindano mbili tu kwa mwaka, kwani hulinda mwili dhidi ya virusi vya UKIMWI kwa kipindi cha hadi miezi sita.

Katika juhudi za kukomesha maambukizi mapya ya virusi vya  UKIMWI , serikali ya Afrika Kusini inapanga kuzindua rasmi dawa hii ya muda mrefu ambayo wataalamu wanasema inaweza kubadilisha mwelekeo wa mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Dokta Aaron Motsoaledi, amefafanua kwamba chanjo hii haibadilishi tiba za walioathirika, bali inawalenga watu walio salama, lakini wako katika hatari ya kuambukizwa virusi hivyo.

''Hii si kwa ajili ya matibabu, bali ni kwa ajili ya kinga. Wale ambao tayari wanaishi na VVU wataendelea na tiba zao za sasa. Chanjo hii ni kwa wale ambao bado hawajaambukizwa, lakini wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI, '' alisema Dokta Motsoaledi.

Katika majaribio ya kliniki, Lenacapavir imeonyesha matokeo ya kuvutia hasa miongoni mwa wasichana ambao ni wazazi , kundi ambalo linaongoza kwa maambukizi mapya barani Afrika.

''Katika majaribio, dawa hii ilionekana kuwa na ufanisi wa asilimia 100. Msichana yeyote anayepokea chanjo hizo mbili kwa mwaka anahakikishiwa ulinzi kamili dhidi ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI, " alieleza Daktari huyo.

Kauli ya WHO kuhusu chanjo hiyo

Kwa upande wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Mkurugenzi Mkuu Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema mafanikio haya yanaweza kuwa hatua muhimu kuelekea kukomesha kwa UKIMWI barani Afrika.

''Japo tunakabiliwa na changamoto nyingi, chanjo hii yenye nguvu ya kinga inaweza kuisaidia Afrika Kusini kufikia lengo lake la kuumaliza UKIMWI,'' alisisitiza Ghebreyesus.

Kwa muda mrefu, hospitali nyingi nchini  Afrika Kusini  zimekuwa zikizidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa UKIMWI, huku wengi wao wakirudi wakiwa na hali mbaya baada ya kusitisha tiba. Ujio wa Lenacapavir unatarajiwa kupunguza mzigo huo, kwa kuwa watu wengi zaidi watafanikiwa kujikinga mapema kabla ya kuambukizwa.

Joseph Nkosi, mkaazi wa Pretoria anazungumzia umuhimu wa chanjo hii, ambapo anasema itasaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

''Dawa hii itawasaidia sana vijana wa Afrika Kusini, na pia itasaidia kupunguza ongezeko la maambukizi mapya, '' alisema mkaazi mmoja wa mji wa Pretoria.

Cha kuvutia zaidi, ni kwamba chanjo hii ambayo hapo awali iligharimu dola elfu 28 za Marekani kwa mwaka, sasa itauzwa kwa dola 40 pekee, chini ya asilimia 0.1 ya bei ya awali. Hili limewezekana baada ya kampuni ya Gilead kutoa leseni za bure kwa wazalishaji wengine, kwa msaada wa mashirika kama Clinton Health Access Initiative na Taasisi ya Gates.

Chanjo inayoleta matumaini makubwa

Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa afya Barani Afrika Limakatso Lebina anasema, kwa sasa hii ndiyo dawa ya kwanza duniani yenye nguvu kubwa dhidi ya UKIMWI:

''Hii ndiyo mara ya kwanza kuona dawa ya  kinga dhidi ya VVU  inayotoa ulinzi wa asilimia 100 kwa wanawake waliochoma sindano. Wote waliotumia hawakuambukizwa, tofauti na wale waliotumia dawa za kumeza kila siku.''

Wataalamu wanasema chanjo hii inaweza kuwa ngao muhimu ya kinga kwa makundi yenye hatari kubwa kama vile wasichana walioko kwenye balehe, vijana wa kike, na wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI , UNAIDS, zaidi ya watu milioni 40 duniani wanaishi na virusi vya UKIMWI. Na iwapo hata asilimia 4 tu ya watu wataanza kutumia sindano hii, inaweza kupunguza hadi asilimia 20 ya maambukizi mapya duniani.

Kwa sasa, Afrika Kusini inasubiri kibali rasmi kutoka kweny Mamlaka ya Bidhaa za Afya, SAPRA, ili kuanza kutoa dawa hii hatua kwa hatua katika hospitali za umma.

Changia Mada hapa(Reply)


image quote pre code