Je, kula haraka haraka ni mbaya kwa afya yako?
Je, unajikuta ukila chakula chako kwa haraka? Unaweza kutamani kupunguza kasi. Hii ndio sababu…
Dk. Sai Krishna Gudi, kutoka Chuo Kikuu cha Manitoba, Canada amefanya utafiti kuhusu madhara ya kiafya ya kula haraka na anaeleza "hakuna uthibitisho unaoonyesha muda usiofaa au unaofaa zaidi wa kula, hasa inategemea aina ya chakula.
"Hata hivyo, mahali fulani kati ya dakika 10 na 20 kwa kawaida zinaweza kutosha kwa kula.
Kwa ujumla, chini ya au sawa na dakika 10 huonwa kuwa ulaji wa haraka na zaidi ya au sawa na dakika 20 huonwa kuwa ulaji wa polepole."
Hata kama huweki muda wa kula, kuna uwezekano utajua kama wewe ni mlaji haraka, asema mtaalamu wa lishe Reema Pillai.
"Jiulize ikiwa unatambua mojawapo ya ishara hizi: Kumaliza milo yako haraka zaidi kuliko wengine wanaokula nawe, kuvimbiwa baada ya kula, kujisikia kushiba baada ya kumaliza, kujisikia kama unataka kula zaidi," hizi zote zinaweza kuwa ishara kwamba wewe ni mlaji haraka.
Je, ni madhara gani yanayoweza kutokea kiafya?
Hili ndilo tunalolisikia zaidi, lakini limekuwa na mjadala mkali.
Utafiti mmoja uligundua kuwa kasi ya kula haikuathiri dalili kwa watu walio na GERD (reflux ya asidi ya muda mrefu).
Hata hivyo, kula haraka sana kunaripotiwa kuwa sababu ya kuvimbiwa na tumbo kujaa gesi.
Pillai anaeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kumeza hewa tunapokula haraka na "hii inaweza kusababisha dalili za kushindwa kusaga chakula... Ingawa kula haraka huchangia kutosaga chakula, mambo mengine kama vile mfadhaiko na uchaguzi wa aina ya chakula, pamoja na matatizo yaliyopo ya usagaji chakula yanachangia."
Aina ya 2 ya kisukari
Hili ni jambo lililomsukuma Gudi, kufanya utafiti. Alitafiti data za ulimwengu halisi kutoka ulimwenguni kote (hadi 2020) akizingatia tu "tafiti za hali ya juu" na matokeo yake, "Uhusiano unaowezekana kati ya kula haraka na hatari ya kupata kisukari cha aina ya 2 ulibainika."
Kwa hivyo kwa nini kula haraka kunaweza kukuweka hatarini zaidi?
Gudi alipata sababu kadhaa.
Kwanza, ikiwa unakula haraka, kuna uwezekano mkubwa wa kula kupita kiasi, hiyo ni kwa sababu inachukua takriban dakika 20 kwa akili zetu kupokea ishara inayotuambia kuwa tumeshiba, kwa hivyo ikiwa unakula haraka unaweza kuishia kula zaidi kabla ya kujua kuwa umeshiba. Ulaji huu unaweza kuongeza viwango vyako vya sukari.
Gudi pia alidokeza utafiti unaoonyesha kwamba ikiwa unakula haraka, kuna uwezekano mkubwa wa 'kutoa vichocheo maalum ... ambavyo hatimaye huongeza upinzani kwa insulini.'
Hata hivyo, anasema Gudi, bado kuna mengi ya kujifunza kuhusu suala hili - hasa unapozingatia kwamba tafiti nyingi ambazo zimechunguza hili kufikia sasa zimeegemea kwenye majibu ya wanaojitolea kushiri utafiti.
"Utafiti unapaswa kuzingatia kutengeneza kipimo cha kawaida cha kasi au programu ya simu janja, ambayo inaweza kusaidia kufuatilia suala hili zaidi.
"Majaribio yaliyodhibitiwa bila mpangilio na masomo ya uingiliaji wa muda mrefu yanahitajika ili kutathmini uhusiano wa sababu na ikiwa kula polepole kunaweza kuzuia ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2," anaongeza.
Kuongezeka uzito
Hili ni jambo ambalo Dk Toshiaki Ohkuma, Chuo Kikuu cha Kyushu, Fukuoka, Japan, amechunguza.
"Mapitio yetu ya utaratibu na uchambuzi, ambao ulijumuisha data kutoka kwa tafiti 23, ulipata uhusiano wazi kati ya kula haraka na kuongezeka kwa uzito wa mwili, ikiwa ni pamoja na uzito uliopitiliza.
"Watu waliokula haraka walikuwa na kiwango cha juu cha uzito wa mwili (BMI) kwa wastani wa 1.78 kg/m² ikilinganishwa na wale waliokula polepole. Zaidi ya hayo, wale wanaokula haraka walikuwa na uwezekano wa kuwa wanene zaidi ya mara mbili, na uwiano wa 2.15.
"Uhusiano huu haukubadilika baada ya marekebisho ya ulaji wa jumla wa nishati. Hii inaangazia umuhimu wa sio tu kile tunachokula na kiasi gani, lakini pia jinsi tunavyokula haraka.
"Kuhimiza ulaji wa polepole kunaweza kuwa mbinu inayofaa ya kuzuia kunenepa kupita kiasi," aeleza Ohkuma.
Sababu za kuongezeka uzito ni sawa na ongezeko linalowezekana la ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2. "Wakati wa kula haraka, watu hutumia kalori zaidi kabla ya ubongo kupokea ishara za utoshelevu, ambazo huchochewa na ulaji wa virutubisho, mshtuko wa tumbo na kutolewa kwa homoni za utumbo.
Ucheleweshaji huu wa kutambua kushiba husababisha kula kupita kiasi, na kusababisha ulaji wa kalori nyingi na kupata uzito zaidi.
"Zaidi ya hayo, wale wanaokula haraka wanaweza kutafuna kidogo, na hivyo kupunguza uanzishaji wa njia zinazohusiana na shibe, na kuchangia zaidi kunenepa kupita kiasi."
Ohkuma anaonya hivi: "Kula haraka kunaweza kusababisha matokeo mengine mabaya kiafya mbali na kunenepa kupita kiasi, kwani kunenepa kupita kiasi ni sababu kuu ya hatari kwa magonjwa mbalimbali sugu, ikiwemo kisukari cha aina ya 2, shinikizo la damu, ugonjwa wa mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na magonjwa ya moyo na mishipa."
Jinsi ya kupunguza kasi ya kula
Mbinu inayoweza kuwasaidia watu ni kula kwa uangalifu. "Ni kukihisi chakula chako kikweli, kuzoea ladha, muundo, harufu na kila hisia inayoletwa na kula," anaeleza Dk. Michael Mantzios, profesa wa saikolojia iliyotumika na ya majaribio katika Chuo Kikuu cha Birmingham City, ambaye amefanya utafiti kuhusu ulaji salama.
"Fikiria hivi. Unafurahia mlo, unazingatia ladha, muundo na/au harufu na ghafla akili yako inatangatanga kwenye orodha ya mambo ya kufanya, tatizo la kazini, au mazungumzo ya hivi karibuni.
Kula kwa uangalifu ni mazoea ya kutambua wakati akili yako inahangaika kwa fikra mbalimbali na kurudisha umakini wako kwenye chakula kilicho mbele yako.
"Iwe ni sauti inayokuvuta mbali au wazo linalokupeleka mahali pengine, kula kwa uangalifu ni uwezo wa kurudisha fikra hapa na sasa, ukifurahia kila hatua kama inavyotokea."
Ingawa lengo kuu la kula kwa uangalifu sio kupungua wakati unakula, ni matokeo.
"Kula kwa uangalifu mara nyingi husababisha kula polepole zaidi ... kwa kawaida hupungua, unasimama ili kufahamu kile unachokula na matokeo yake, unachukua muda wako.
Kwa hiyo, wakati kula polepole hutokea kwa kuzingatia na kula kwa uangalifu, sio jambo ambalo unapaswa kulazimisha; huja tu kwa kawaida unapozingatia zaidi uzoefu wa hisia."
Ufanyeje?
"Jaribu mazoea rahisi ya kutafakari wakati wa kula—weka kipande cha karatasi karibu na sahani yako na uandike chini ukumbusho wa kile unachohitaji kutambua: ladha, harufu, au muundo wa chakula chako. Inaweza kuwa rahisi kama: Je! ni ladha gani? Harufu ikoje? Kimeandaliwaje kwa vitu gani?
"Huna haja ya kuandika chochote wakati unakula, iwe tu kama ukumbusho wa kile unachozingatia wakati wa chakula.
"Akili yako ikitangatanga, ni sawa - jikumbushe tu kuzingatia tena uzoefu wa hisia na bila kujali ni mara ngapi hutokea, rudia mzunguko huu kutakufanya uwe mlaji makini zaidi."
Usisite kupata ushauri wa mtaalamu wako wa afya inapobidi.
Reply
image quote pre code