Ticker

6/recent/ticker-posts

Vijana barubaru kukabiliwa Zaidi na changamoto ya Afya ya Akili - WHO



Vijana barubaru kukabiliwa Zaidi na changamoto ya Afya ya Akili - WHO

Kwa mujibu wa Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) uwekezaji wa haraka unahitajika ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoongezeka kwa vijana barubaru ikiwemo kuhakikisha mahitaji ya afya ya akili pamoja na afya ya uzazi kwa vijana bilioni 1.3 duniani kote yanatimizwa. Kulingana na ripoti hiyo, ujana ni hatua ya kipekee na muhimu katika maendeleo ya binadamu, ambapo misingi ya afya bora ya muda mrefu huwekwa.

"Kuhamasisha na kulinda afya na haki za vijana ni muhimu kwa kujenga mustakabali bora kwa dunia yetu," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus huku akionya kuwa kushindwa kushughulikia vitisho vya kiafya vinavyowakabili vijana  baadhi vikiwa vimekuwepo kwa muda mrefu na vingine vikiwa vipya kutaleta athari kubwa kwa vijana wenyewe na kusababisha gharama kubwa kwa jamii. "Hii inafanya uwekezaji katika huduma na programu za afya ya vijana kuwa si tu jambo la kimaadili bali pia ni jambo lenye maana kiuchumi," ameongeza.

Ripoti hiyo Mpya imezinduliwa hivi karibuni ikiwa kuna mkutano wa mustakabali wa Umoja wa Mataifa na imebainisha uwepo wa wasiwasi kwenye afya ya vijana kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, ikionesha hitaji la hatua za haraka.

Takribani kijana mmoja kati ya vijana 7 duniani wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili kama vile unyogovu(depression) na wasiwasi(anxiety). Aidha, kiwango cha upungufu wa damu kwa wasichana vijana hakijabadilika tangu mwaka 2010, huku karibu kijana mmoja kati ya vijana 10 wakiwa wanakabiliwa na Unene kupita kiasi.

Maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs), ikiwa ni pamoja na;

  • kaswende,
  • klamidia,
  • Pamoja na virusi vinavyosababisha malengelenge sehemu za siri,

yanazidi kuongezeka, hali ambayo inahitaji tiba mapema ili kuepusha athari za muda mrefu kwa afya.

Vile vile, ghasia, ikiwemo uonevu, huathiri mamilioni ya vijana kila mwaka, na kuwa na athari mbaya kwa afya zao za kimwili na kiakili.

Wasiwasi kuongezeka:

Wasiwasi umeongezeka zaidi, Kwani vizuizi vinavyosababisha vijana kutokupata huduma za afya ya uzazi vimeongezeka, huku Sera Zinazoboresha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya zinaa na VVU kwa vijana zikiendelea kutelekezwa. Hatua hizi zinapunguza mwitikio wa vijana kutafuta huduma, hali inayosababisha athari za kiafya za muda mrefu.

Ripoti hiyo pia inasisitiza changamoto nyingine kubwa zinazokabili mustakabali wa vijana, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, migogoro, na ukosefu wa usawa. Hata hivyo, waandishi wa ripoti hiyo wamebainisha kuwa mafanikio yanawezekana kupitia uwekezaji sahihi na msaada.

Mafanikio kama vile kupungua kwa maambukizi ya VVU miongoni mwa vijana, kupungua kwa mimba za utotoni, na kupungua kwa vitendo vya ukatili kama vile ukeketaji na ndoa za mapema ni matokeo ya juhudi za pamoja. Aidha, ongezeko la wasichana wanaosalia shuleni limechangia katika kuboresha afya za vijana, na tangu mwaka 2000, idadi ya watoto wenye umri wa kwenda sekondari wasio shuleni imepungua kwa karibu asilimia 30.

Wito wa ripoti hiyo

Kwa kuzingatia changamoto hizi, ripoti hiyo inatoa wito wa uwekezaji zaidi katika afya na ustawi wa vijana, kwa kuzingatia masuala ya elimu, huduma za afya, na lishe bora. Waandishi wanasisitiza umuhimu wa kuweka sheria na sera zinazolinda haki za vijana, huku mifumo ya afya ikitakiwa kuwa rafiki kwa mahitaji yao maalumu.

"Vijana wana uwezo mkubwa wa ubunifu wanapopewa fursa ya kushiriki katika maamuzi kuhusu ustawi wao na mustakabali wao," amesema Rajat Khosla, Mkurugenzi Mtendaji wa Ushirikiano wa Afya ya Mama, Watoto wachanga, na Watoto (PMNCH) na kuongeza kuwa "Viongozi lazima wasikilize sauti za vijana na kuhakikisha wanakuwa washirika muhimu katika maamuzi."

Viongozi wa dunia, katika mkutano wa Afya Duniani mwaka huu, wameahidi kuongeza juhudi za kuboresha afya ya vijana, ikiwa ni sehemu ya ahadi zao katika mkataba wa mustakabali wa Umoja wa Mataifa. Utekelezaji wa ahadi hizi utakuwa muhimu katika kulinda na kuboresha afya na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Source Credits|Link; Via

United Nations(UN)

Shirika la Afya Duniani(WHO)

Afyaclass(Reviewed&edited)



Post a Comment

0 Comments