UNAIDS inakadiria kutatokea maambukizi mapya ya VVU milioni 6 na vifo vya ziada ya milioni 4 kati ya 2025 na 2029

UNAIDS inakadiria kutatokea maambukizi mapya ya VVU milioni 6 na vifo vya ziada ya milioni 4 kati ya 2025 na 2029

#1

Shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na UKIMWI, UNAIDS leo limezindua ripoti yake ya mwaka huu wa 2025 ya hali ya Ugonjwa wa UKIMWI. “UKIMWI, Janga  na mabadiliko,” inayoonesha kuwa kuna janga kubwa la kifedha linalotishia kuvuruga mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa, isipokuwa mataifa yatekeleze mabadiliko makubwa katika programu na ufadhili wa ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi, VVU, Imesema ripoti iliyotolewa leo na Shirika hilo la UNAIDS mjini Geneva Uswisi na Johannesburg, Afrika Kusini.



Ripoti hiyo inasisitiza athari za ghafla za upunguzaji mkubwa wa ufadhili kutoka kwa wafadhili wa kimataifa, hasa katika nchi zilizoathirika zaidi na VVU. Hata hivyo, inatoa mifano ya kuhamasisha ya nchi na jamii ambazo zimeonesha uimara kwa kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI licha ya changamoto kubwa.

Kati ya nchi 60 za kipato cha chini na cha kati zilizojumuishwa katika ripoti, 25 zimeonesha nia ya kuongeza bajeti zao za ndani kwa ajili ya kukabiliana na VVU ifikapo 2026. Ongezeko hili linakadiriwa kuwa la asilimia 8, sawa na takribani dola milioni 180 za Kimarekani — hatua nzuri lakini bado haitoshi kufidia upungufu wa ufadhili wa kimataifa katika nchi zinazoitegemea pakubwa.

Janga la kimataifa: Upungufu mkubwa wa fedha watishia kurejesha nyuma mafanikio

Licha ya mafanikio yaliyoonekana katika mwaka wa 2024, kupungua kwa misaada ya kimataifa na upungufu mkubwa wa fedha katika mwaka wa 2025 umesababisha machafuko katika mifumo ya afya, kukatiza huduma za msingi za afya, na kupunguza huduma za kinga na tiba dhidi ya VVU.

Nchini Msumbiji pekee, zaidi ya wahudumu wa afya 30,000 wameathirika. Nchini Nigeria, idadi ya watu wanaoanza kutumia dawa za kuzuia maambukizi ya VVU (PREP) imeshuka kutoka watu 40,000 hadi 6,000 kwa mwezi. Ikiwa huduma zinazofadhiliwa na Marekani zitakoma kabisa, UNAIDS inakadiria kutatokea maambukizi mapya ya VVU milioni 6 na vifo vya ziada ya milioni 4 kati ya 2025 na 2029.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima anasema, “Hii si pengo la kifedha tu -ni bomu linalosubiri kulipuka. Tumeona huduma zikisimama ghafla. Wahudumu wa afya wamerejeshwa nyumbani. Na watu, hasa watoto na makundi muhimu wakikosa huduma.”

Tayari kufikia 2024, watu milioni 9.2 waliokuwa wakiishi na VVU hawakuwa wakipata dawa za kuokoa maisha. Miongoni mwao, watoto 620,000 wenye umri wa miaka 0 hadi 14 hawakupata tiba, na kusababisha vifo vya watoto75,000.

Watu 630,000 walifariki dunia kutokana na UKIMWI, asilimia 61 kati yao wakiwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Wasichana balehe na wanawake vijana zaidi ya 210,000 wenye umri wa miaka 15–24 waliambukizwa ugonjwa wa VVU mwaka huo, wastani wa maambukizi mapya 570 kwa siku.

Huduma za kinga dhidi ya VVU zimevurugika pakubwa. Huduma zinazoendeshwa na jamii, ambazo ni muhimu kwa makundi ya pembezoni, zimekosa ufadhili kwa kasi ya kutisha. Mapema 2025, zaidi ya asilimia 60 ya mashirika ya wanawake yanayotoa huduma za VVU yalikuwa yamepoteza ufadhili au kulazimika kusitisha huduma zao.

Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) ulifikia wasichana na wanawake vijana milioni 2.3 wenye huduma za kina za kuzuia VVU mwaka 2024 na kuwezesha watu milioni 2.5 kutumia VVU PrEP, lakini programu hizi sasa zimeacha kabisa.

Wakati huo huo, ongezeko la sheria kandamizi dhidi ya mahusiano ya watu wa jinsia moja, utambulisho wa kijinsia, na matumizi ya dawa za kulevya limezidisha janga hili kwa kufanya huduma za VVU kutopatikana kwa watu wanaozihitaji zaidi. Nchi kama Uganda, Mali na Trinidad na Tobago zimeona mabadiliko ya hivi majuzi yenye madhara na ya ubaguzi kwa sheria zao za uhalifu zinazolenga watu muhimu, na kuwasukuma mbali zaidi kutoka kwa matunzo na kuongeza hatari yao ya kupata VVU.

Tumaini lipo: Nchi na jamii zinaibuka kulinda mafanikio ya tiba ya VVU

Afrika Kusini kwa sasa inafadhili asilimia 77 ya mapambano yake dhidi ya UKIMWI, na katika mapitio ya bajeti ya 2025, imepanga kuongeza bajeti ya afya kwa asilimia 5.9 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 3 ijayo, ikiwa ni pamoja na asilimia 3.3 ya ongezeko la mwaka kwa programu za VVU na kifua kikuu. Serikali pia inanuia kuanzisha mfumo wa taarifa za wagonjwa, mfumo wa usambazaji wa dawa za muda mrefu, na mfumo wa ufuatiliaji wa akiba ya dawa katika vituo vya afya.

Kufikia Desemba 2024, nchi 7 — Botswana, Eswatini, Lesotho, Namibia, Rwanda, Zambia, na Zimbabwe,  zilikuwa zimefikia malengo ya 95-95-95: asilimia 95 ya watu wanaoishi na HIV wanajua hali yao, asilimia 95 ya hao wapo kwenye matibabu, na asilimia 95 ya waliopo kwenye tiba wana kiwango kidogo cha virusi mwilini.

Ripoti pia inaangazia matumaini mapya kupitia zana za kisasa za kuzuia maambukizi kama vile PrEP ya sindano ya muda mrefu kama Lenacapavir, iliyothibitishwa kuwa na ufanisi mkubwa katika majaribio ya kitaalamu , ingawa changamoto za upatikanaji na bei bado ni kubwa.

Bado kuna nafasi ya kugeuza janga hili kuwa fursa. Nchi zinaongeza fedha za ndani. Jamii zinaonesha mbinu zinazofanya kazi. Sasa tunahitaji mshikamano wa kimataifa kuunga mkono ujasiri wao.” amesema Bi. Byanyima

Wito wa mshikamano

Ripoti ya UNAIDS ya 2025 inahitimisha kwa wito wa dharura. Mapambano dhidi ya VVU hayawezi kutegemea rasilimali za ndani pekee. Jumuiya ya kimataifa lazima ijitokeze kufidia pengo la ufadhili, kusaidia nchi kufikia malengo ya kinga na tiba, kuondoa vikwazo vya kisheria na kijamii, na kuziwezesha jamii kuongoza njia.

UNAIDS inasisitiza kwamba kila dola inayowekezwa katika kupambana na VVU si tu kwamba inaokoa maisha, bali pia inaimarisha mifumo ya afya na kuchangia malengo mapana ya maendeleo. Tangu mlipuko wa ugonjwa huu uanze, vifo 26.9 milioni vimeepushwa kupitia tiba, na watoto milioni 4.4 wamelindwa dhidi ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Bi. Byanyima anasema,  “Katika wakati huu wa janga, ulimwengu lazima uchague mabadiliko badala ya kurudi nyuma. Kwa pamoja, bado tunaweza kukomesha UKIMWI kama tishio kwa afya ya umma ifikapo 2030, kama tutachukua hatua sasa, kwa mshikamano na dhamira thabiti bila kuyumbayumba."

Related Discussions

REPLY HAPA


image quote pre code