Umri wa Wazee ni moja ya kihatarishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza

Umri wa Wazee ni moja ya kihatarishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza

#1

Kwa Tanzania na nchi nyingine duniani umri wa uzee ni miaka 60 kuendelea. Kitabibu umri huu ni moja ya kihatarishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza.



Sababu ya kimsingi ni kutokana na mchanganyiko wa mambo kadhaa ya kibailojia kama vile kutumika na kulika hatimaye kuchakaa kwa viungo, mrundikano wa mambo hatarishi kiafya kadiri umri unavyoenda na uchaguzi usiofaa wa mitindo ya kimaisha.

Magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuathiri ubora wa maisha ya wazee, kuathiri ustawi wao wa kimwili na kiakili, uhuru na tija.

Ni Changamoto kutibu magonjwa haya kwasababu yanahitaji huduma ziinazoendelea kwa muda mrefu. Hivyo kusababisha kuongezeka kwa gharama kwa mzee binafsi, familia na mifumo ya huduma za afya.

Magonjwa yasiyoambukiza huwapata wazee na hatimaye kufariki au kupata ulemavu wa kudumu na maisha bora ya uzeeni.

Ni kweli umri wa uzee ni kihatarishi cha kupata magonjwa, lakini mzee mwenye mitindo mibaya kimaisha yupo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa haya.

Mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ni pamoja unywaji pombe, uvutaji tumbaku, ulaji holela wa chumvi, sukari, wanga na mafuta na kutofanya mazoezi au kuushughulisha mwili na kazi.

Magonjwa hayo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, unene, matatizo ya mishipa ya damu ya moyo, lehemu nyingi, kiharusi na kisukari.

Vile vile ugonjwa sugu wa figo, matatizo sugu mfumo wa hewa, saratani mbalimbali, matatizo ya viungo vya mwili ikiwamo mifupa na magonjwa ya akili.

Ni muhimu kutumia njia za kujikinga mapema kabla ya kupata magonjwa hayo, hasa kwa wale wanaoelekea uzeeni, ambao tayari ni wazee au tayari wanakabiliwa na magonjwa hayo.

Hatua muhimu kujua huduma za afya zilizopo jirani na anapoishi ili iwe rahisi kupata ushauri wa kiafya hata kabla ya kuugua.

Mazingira bora ya kuishi yasiyo katika mazingira yenye uchafuzi wa hewa na kelele nyingi, lishe bora iliyozingatia kanuni za afya na mazoezi mepesi ni muhimu kwa afya ya wazee.

Wazee walio katika hatari ya kupoteza maisha mapema wanapopata magonjwa hayo ni wale wa nchi za kipato cha chini mpaka kati. Wengi wao hawana uwezo wa kufanya kazi ngumu za kujiingizia kipato.

Vile vile tayari wameisha staafu kazi zile walizokuwa wameajiriwa na pengine alikuwa na bima kubwa ya afya lakini sasa huenda hana au anayo lakini ni ya kawaida.

Umri wa miaka 60+ wanatakiwa kupendelea zaidi kula mlo mboga mboga, matunda, protini itokanayo na mimea, kuepuka chumvi, sukari au wanga na mafuta mengi.

Vyema umri huo kuwaona wataalam lishe katika huduma za afya ili kukupa mwongozo mpana na ratiba ya vyakula.

Mzee kufanya mazoezi huwa ni vigumu, kwa yule anayeweza kutembea vyema kufanya zoezi la kutembea angalau hatua 10,000 kwa siku au umbali wa kilometa 2 kwa dakika 30 kwa siku katika siku 5 za wiki.

Au kujishughulisha na kazi za nyumbani kama kazi bustani au usafi wa nyumba na mazingira unaweza kutumia kama mazoezi au anayeishi mazingira rafiki kwa kutembea.

Kulala angalau saa 8 kwa usiku mmoja, kupata mapumziko na kupata burudisho ili kuepukana na matatizo ya akili.

Angalau kufanya uchunguzi wa afya wa jumla mara moja kwa miezi 6, hii inasaidia kubaini matatizo ya kiafya mapema kwa gharama ndogo.

Kuwepo kwa ongezeko la vihatarishi vinavyochangia kutokea kwa matatizo hayo, ni muhimu wazee kushikamana na njia za kujikinga mapema kabla ya kuugua.

Kwa wanaotarajia kuelekea umri wa uzeeni kuanza kuchukua hatua hizi mapema na pia kuwekeza katika afya zao ikiwamo kuwa na bima za afya.

 By DK. SHITA SAMWEL

REPLY HAPA


image quote pre code