Mafuriko ya ghafla yaikumba Somalia,Zaidi ya Watu 45,000 waathirika
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema mafuriko ya ghafla yaliyokumba Somalia tangu tarehe 15 mwezi uliopita yamesababisha uharibifu mkubwa huku zaidi ya watu 45,000 wakifurushwa makwao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani Jana Ijumaa, Dujarric amenukuu watendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya dharura, OCHA wakisema mamlaka za Somalia zimeripoti vifo kutokana na mafuriko hayo, miongoni mwao wakiwa ni watoto.
Kufurika kwa mto Shabelle
Tarehe 28 mwezi uliopita wa Aprili ,mto Shabelle katika wilaya ya Jowhar jimboni Hirshabelle ulifurika na kusababisha zaidi ya wakazi 6,000 kukimbilia maeneo ya nyanda za juu ili kujihifadhi.
Katika Jimbo la Galmudug, mafuriko ya ghafla katika sehemu za mji wa Gaalkacyo yamesababisha madhara kwa zaidi ya watu 9,500 ambao tayari ni watu waliokimbia makazi yao wanaoishi katika makazi ya muda.
Dujarric amesema janga hili linatokea wakati mashirika ya kibinadamu, hasa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitaifa, yanakabiliwa na upungufu mkubwa wa ufadhili. “Makundi mengi yamelazimika kusitisha, kupunguza au hata kumaliza kazi zao muhimu wanazofanya kwenye eneo,” amesema Dujarric.
Theluthi moja ya watu Somalia wanahitaji msaada
Kwa sasa, takriban theluthi moja ya idadi ya watu wa Somalia, sawa na takribani watu milioni 6, wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Amesema licha ya ombi la kibinadamu la dola bilioni 1.4, wahudumu wa kiutu tumepokea dola milioni 148 tu hadi sasa, ambayo ni takriban asilimia 10 ya fedha zinazohitajika.
Dujarric amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa ili kushughulikia changamoto zinazoendelea kuongezeka na wakati huo huo kutoa msaada unaohitajika kwa watu walioathirika.
Reply
image quote pre code